NA TATU MAKAME
MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Uhifadhi na uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar, Madina Haji Khamis, amewahakikishia wananchi watakaopisha ukarabati katika mji huo kuwa watarejeshwa mara harakati za ukarabati utakapomalizika.
Alisema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Kikwajuni Wilaya ya mjini, ambapo alisema lengo la serikali ni kuona majengo hayo yanakuwa katika haiba nzuri na sio kuwaondosha wananchi na kuwapeleka katika maeneo mengine.
Alisema serikali imeona pana haja ya kufanya ukarabati wa nyumba hizo kutokana na ubovu, ili kuyanusuru yasianguke hivyo aliwahakikishia wananchi wanaoishi katika nyumba hizo kuwa watarejeshwa katika makaazi yao hapo baadae.
Alieleza kwamba Mjimkongwe ndio sehemu yenye kuongeza pato kubwa la taifa na mtu mmoja mmoja, hivyo uamuzi wa serikali wa kuyafanyia ukarabati majumba hayo unafaa kuungwa mkono.
Alifahamisha kuwa zaidi ya nyumba 120, ambazo zinahitaji kufanyiwa ukarabati na majengo mengine yapo katika hatari ya kuanguka.
“Tumeona kuwa hata miundombinu yake hairidhishi hivyo kutokana na umuhimu wa majumba haya tunaona ipo haja ya kufanyia ukarabati wa miundombinu ikiwemo maji na umeme”, alisema.
Mkurugenzi huyo, aliwataka wananchi wazalendo na wale wanaoishi nje ya nchi kujitokeza kwenye maombi ya ukarabati wa majumba hayo na kuacha kuwategemea wageni pekee kufanya kazi ya ukarabati kwani fursa ya ukarabati inatolewa kwa watu wote.
Sambamba na hayo, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itashirikiana kwa karibu na watu wanaotaka kutoa majumba yao kwa ukarabati wa majumba ya Mji huo, ambao ni urithi wa taifa kwa kuyaongezea hadhi na kudumu kwa muda mrefu.
Nao wananchi wanaokaa katika Mjimkongwe waliipongeza serikali kwa uamuzi wao wa kuyafanyia ukarabati majumba hayo na kusema wako tayari kuondoka endapo kutakuwa na mikataba ya uhakika wa kurejeshwa kwenye nyumba zao mara ukarabati utakapomalizika.