Amaliza mchakato wa uwekezaji

NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

MWEKEZAJI wa klabu ya Simba na Mwenyekiti  wa Bodi ya Wakurugenzi  klabu hiyo , Mohammed Dewj, amekabidhi shilingi Billioni 20 ya hisa asilimia 49 za klabu hiyo mbele ya  Mdhamini wa klabu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilisha mchakato wa mabadiliko na kupata hati kutoka FCC ya kuwaruhusu kumaliza mchakato.

Hundi ya pesa hizo ilikabidhiwa jana kwenye mkutano wa waandishi wa Habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mkutano huo MO Dewj alianza kwa kuwashukuru watu wote, ambao wamehusika kwenye mafanikio ya Simba kuanzia wadhamini, viongozi wa Bodi na watu ambao wapo nyuma yapazia lakini wanaipambania Simba.

Siri ya mafanikio ambayo yamewafikisha hapo kwenye miaka minne ni  nidhamu, kuweka maslahi ya timu mbele umoja na maelewano baina yetu.

Alisema katika mafanikio ambayo Simba wameyafika leo hii ameshatumia Bilioni 21.3 zaidi ya ambao anatakiwa kuweka, na imetumika kwa kufanya usajili, ‘pre season’, mishahara pamoja na mambo mengine ya klabu, lakini hiyo yeye ameitoa tu kwa sababu anaipenda Simba.

“Tumekamilisha mchakato wa mabadiliko na tumepatiwa hati na FCC ya kukamilisha mchakato, hivyo leo nina weke Bilioni 20 ya hisa asilimia 49 mbele ya klabu na mdhamini wa klabu,” alisema MO Dewj