NA KHAMISUU ABDALLAH

KAMPUNI tanzu ya Kampuni ya Vigor kampuni International Limited, V- Cleaning Company Limited inatarajia kufanya majaribio ya ukusanyaji kwa kubagua takataka kwa kutumia mifuko maalum.

Meneja wa kampuni hiyo Julius George, aliitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Zanzibar leo ofisini kwake Migombani Mjini Unguja na kueleza kuwa hatua hiyo imelenga kuzifanya taka kuwa mali na itahusisha nyumba za mjini pekee.

Alisema pia hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kudhibiti taka na wataanza majumbani na katika maeneo ya huduma za kijamii au biashara.

Alidha alisema mfumo huo utahusisha kuwa na mifuko ya aina ya tatu ikiwemo rangi ya Manjano, Kijani na Nyeusi, ambayo imeshaatengenezwa kupitia kiwanda cha Turky na wanataka kuiwasilisha Baraza la Manispaa Mjini kwa ajili ya kupata vigezo vya kutumika majumbani kwa ajili ya uhifadhi wa taka za aina tatu tofauti.

“Lengo letu kuweka mfumo huu mzima wa kutunza taka kwa kuondokana na dhana ya awali ambayo ilikuwa ni kukusanya taka na kutupa kwa kuja na falsafa mpya ambayo inahusisha kukusanya kubagua na kuzirejesha katika hali ya matumizi ya mwanzo colaction, segregation risaitle,” alibainisha.

Alisema baada ya kumaliza zoezi hilo itatoa ripoti kwa wananchi na kuzindua mifuko hiyo rasmi ili iweze kutumika kwa kushirikiana na Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed kwani ni mkakati mmoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumzia lengo lao kuingia mkataba na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni kuhakikisha inasimamia maeneo yote yanakuwa masafi kwa kuhakikisha taka ngumu na taka zinazooza zinahifadhiwa vizuri na zinatunzwa ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira hasa katika mji wa Zanzibar ambao ndio kitovu cha Mji unaotizamwa na mataifa mengi yanayokuja kwa njia mbalimbali ikiwemo utalii.

Aidha alisema mikakati yao katika suala la kusimamia usafi ni kuhakikisha taka haziwi kikwazo katika kuleta madhara kwa wananchi hasa maradhi ya mripuko ikiwemo kuharisha.

“Zanzbar ina kilomita za mraba 2,464 huku zaidi ya 300 zikiwa katika mkoa wa Mjini Magharibi na asimilia ya taka zinazokusanywa kila siku ni tani tano kwa kapu moja na ili kukabilian na changamoto ya uchafu zinahitajika kufikia tripu 30 kwa siku,” alieleza.