NA DORINA MAKAYA – KATAVI
NAIBU Waziri wa Nishati, amefanya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme vijijini Awamu ya III Mzunguko wa pili katika kijiji cha Ilangu, kata ya Ilangu, tarafa ya Kabungu, wilaya ya Tanganyika, mkoa wa Katavi.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Naibu Waziri Byabato amesema, zaidi ya shilingi bilioni 15 zitatumika kuvipelekea umeme vijiji 25 vya wilaya ya Tanganyika, ambapo alisema, kwa kijiji cha Ilangu peke yake, takriban shilingi millioni 618 zitatumika kuunganisha umeme.
Amesema, serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji umeme nchi nzima na kuwa upatikanaji wa umeme vijijini utachangia kuongezeka kwa kasi ya uanzishwaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao na kuwa kichocheo cha ukuaji wa biashara na uchumi kiujumla.
Naibu Waziri Byabato, amewaambia wanakijiji cha Ilangu kuwa, Serikali imewapunguzia wananchi gharama ya kuunganishiwa umeme kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000 tu kwa wateja wa umeme wa njia moja na kwa wateja wa umeme wa njia tatu kutoka shilingi 912,000 hadi shilingi 139,500 ili kuwawezesha wananchi kuunganishiwa umeme.
Amesema, kwa mwananchi ambaye atakuwa hajakamilisha kupata pesa kamili za kulipia anaweza kulipa kidogo kidogo ndani ya kipindi cha Mradi wa eneo husika na atakapokamilisha ataunganishiwa umeme.
Naibu Waziri Byabato, amemtaka mkandarasi wa Mradi kuhakikisha anawaunganishia umeme wateja wote bila kujali aina ya nyumba anayoishi na kutoa kipaumbele kwa taasisi na maeneo yanayotoa huduma za kijamii kama vile vituo vya afya, shule, nyumba za ibada, ofisi za Serikali, visima vya maji pamoja na viwanda vidogo ambavyo vitachangia kasi ya maendeleo katika eneo husika na Taifa kiujumla.