NA BAKAR MUSSA, PEMBA

MRATIBU wa uchaguzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi Pemba, Latifa Mohammed Makame, amevipongeza vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la Konde kwa kufanya kampeni za kistaarabu.

Mratibu huyo alieleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, huko Kisiwani Pemba kuhusiana na kampeni zilivyoendeshwa na matayarisho ya uchaguzi wa ubunge unaotarajiwa kufanyika leo.

Alisema kampeni kwenye uchaguzi wa jimbo la Konde unaofanyika leo zimefanyika kistaarabu, pia zilifanyika kwa amani na utulivu na kuwataka wananchi wa Konde kuendelea kudumisha hali hiyo wakati na baada ya kupiga kura.

Akizungumzia matayarisho ya uchaguzi huo, alieleza kuwa kila kitu kimekamilika ikiwemo matayarisho ya vituo vya kupigia kura sambamba na upokeaji wa vifaa.

“Matayarisho yote ya uchaguzi wa leo yamekamilika na tunachokisubiri ni kwa zoezi hili muda utakapowadia,” alisema.

Latifa, aliwataka wananchi wa jimbo la Konde kujitokeza kwa wingi kuchagua kiongozi wanayempenda kwa wakati katika vituo 16 vilivyotayarishwa kwa ajili ya zoezi hilo.

Alifahamisha kuwa vituo vyote vitafunguliwa saa 1 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni kama kawaida ya chaguzi zote sambamba na kufuata taratibu zote za uchaguzi zilizowekwa na sheria.

“Sheria zitakazotumika kwa uchaguzi huu mdogo wa jimbo la Konde ni zile zile zilizotumika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita, vituo tutavifungua saa 1 asubuhi na kufungwa saa 10 alaasiri”, alisema

Mratibu huyo aliwataka wapiga kura wa jimbo hilo kutokukubali kushawishiwa kujiingiza katika uchafuzi wa amani katika kipindi cha uchaguzi utakapofanyika na utakapomalizika wananchi warudi nyumbani kusubiri matokeo.

Vyama vilivyoshiriki uchaguzi wa leo kuwania kiti cha ubunge ni pamoja na CCM, ACT Wazalendo, CUF, ADA TADEA, NCCR, CHADEMA, SAU, NRA, UPDP, DEMOKRASIA MAKINI, CCK.