NA MADINA ISSA

MKUU wa Divisheni ya takwimu za watoaji huduma katoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Bakari Khamis Kondo, amesema hali ya biashara kwa mwezi Mei mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 53.8 ikilingaishwa na mwezi Mei mwaka 2020 huku ikipungua kwa asilimia 15.0 ukilinganisha na mwezi Aprili mwaka huu.

Aliyasema hayo alipokuwa akitoa tathmini na mwenendo wa hali ya biashara kwa mwezi wa Mei mwaka huu huko Ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja.

Alisema mwenendo wa biashara bado unaendelea kuwa katika hali nzuri na kuongezeka kwa asilimia 53.8 ukilinganisha na mwezi Mei mwaka jana.

Aidha, alisema, hali hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali, na kusema kwa makadirio ya fedha ni bilioni 70.5 huku thamani nzima za bidhaa zilizosafirishwa kutoka Zanzibar kwenda nje ya nchi zilikuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.9.

“Kwa thamani ya bidhaa zilizosafirishwa zimeongezeka kwa asilimia 8.4 ikilinganishwa na mwezi Mei 2020 na kwa asilimia 19.5 ukilinganisha na mwezi Aprili 2021,” alieleza.

Hata hivyo, alisema kuwa bidhaa zilizosafirishwa ni pamoja na chakula, wanyama hai bidhaa zilizotengenezwa aina ya malighafi, vifaa ghafi vya nishati ya mafuta, mashine na vifaa vya usafirishaji, bidhaa za viwandani pamoja na kemikali.

Sambamba na hayo, alisema kwa upande wa usafirishaji wa bidhaa kwa nchi tano bora kwa mwezi Mei mwaka huu umefikia asilimia 70.6 ya bidhaa zote zilizosafirishwa.

“Nchi ya Denmark imeongoza kwa kusafirisha bidhaa zenye thamani ya shilingi 620 milioni sawa na asilimia 21.0,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema kuwa katika nchi nyengine zinazoongoza katika usafirishaji wa bidhaa ni Vietnam, China, India na Uganda ambapo bidhaa kuu zilikuwa mwani, pumba, samaki aina ya kaa, kamba pamoja na makobe.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa Zanzibar kwa mwezi Mei mwaka huu bidhaa zilizosafirishwa nje ya nchi zilikuwa nguo za mitumba, vyuma chakavu, vitenge, kanga na vikoi ambapo bidhaa zilizoagizwa kwa mwezi Mei mwaka huu zina thamani ya shilingi bilioni 73.5.