IMETAYARISHWA NA MAALIM OMAR MUSSA HAJI
KATIKA makala hii tutaangalia namna mtazamo wa Dini ya Kiislamu kuhusiana na suala zima la tiba ambapo mtu hutolewa kiungo fulani na Kupandikizwa katika kiwiliwili cha mtu mwengine kwa lengo la kumpa uzima kutokana na maradhi fulani, ili kiungo hicho kichukuwe nafasi ya kiungo kama hicho ambacho kimeathirika .
UTANGULIZI :
Katika kulizungumzia suala hili, ni vyema kwanza kutathmini na kuelewa kuwa wakati huu tulionao zaidi ya watu 105,000 ndani ya bara la Amerika wanasubiri kupatiwa viungo mbali mbali vya mwili ili vipandikizwe katika viwiliwili vyao.
Na kila siku zaidi ya watu 4,000 wanaongezeka katika orodha hiyo. Kila mmoja miongoni mwa watu hao ama anahitaji figo, ini, moyo au kiungo kingine chochote.
Zaidi ya watu 6,500 kwa mwaka sawa na watu 18 kwa siku wanafariki dunia kabla ya kupatiwa viungo hivyo.
Watu wanaochangia kutoa viungo hivyo ni wachache kulinganisha na idadi ya wale wanaohitaji. Mara nyingi viungo vingi vinavyopatikana huwa vinatokana na viwiliwili vya watu waliokwisha fariki dunia. Ni idadi ndogo tu ya viungo hupatikana kutoka kwa watu walio hai na wenye afya.
Kwa mujibu wa takwimu kila mwaka hupandikizwa karibu viungo 6,000 kutokana na watu walio hai. Hata hivyo kuna masuali ya kujiuliza kabla ya mtu kuchangia kiungo chake kwa kumpa mtu mwengine.
NANI ANAWEZA KUCHANGIA KIUNGO CHA MWILI WAKE
Kila mtu katika umri wowote ule anaweza kuchangia kiungo. Lakini yule ambae umri wake uko chini ya miaka 18, anahitaji kupata ridhaa ya wazazi au walezi wake.
Kwa mchangiaji kiungo ambae amefariki ni lazima madaktari wahusishwe katika kuona ni kiungo gani kinafaa na kupandikizwa kwa mtu mwengine, kwani magonjwa kama ukimwi (HIV), kansa yenye kuzagaa au maambukizi yoyote makubwa yanaondoa uwezekano wa mtu kuchangia kiungo.
Kwa hivyo mtu anaeishi pindipo ana maradhi kama ya ukimmwi, kisukari au ugonjwa wa moyo huzuilika asichangie kiungo chake kumpa mtu mwengine.
Jee kuwa na damu ya aina moja (blood group) au nyama ya mwili (Tissues) yenye muundo na kiwango chenye kufanana kati ya mchangiaji na yule anaechangiwa kuna umuhimu kwa mchangiaji kiungo na yule anaepewa.
Itakuwa ni rahisi kwa wawili hao baada ya madaktari kuwapima na kuthibitisha kuwa wana hali inayofanana.
Hata hivyo baadhi ya vitengo vinavyohusika na tiba vinaweza kupandikiza viungo hata kama wawili hao hawafanani katika damu na nyama ya mwili kama tulivyotangulia kusema.
Limekuwa ni jambo la kawaida katika ulimwengu huu kufanyika tiba ya kupandikizwa viungo vya mwili wa mwanadamu ambavyo vimetolewa kutoka katika mwili wa mtu mwengine, kama vile figo na kadhalika.
Jee nini mtazamo wa wanazuoni wa Kiislamu na wanasheria kuhusiana na suala hili. Tukiangalia tutaona kwamba kuna ikhtilafu au mitazamo tofauti kuhusiana na jambo hili, kama inavyoonekana katika vitabu vya (Fiqhi) yaani sheria ya Kiiislamu kama ifuatavyo:-
Endapo kiungo kimetolewa katika mwili wa maiti ambae mwenyewe ameusia au alitoa ruhusa hiyo kabla ya kufariki kwake basi (inasihi) inakubalika kisheria kutolewa kiungo hicho kwa kuwa hakuna (dalili) ushahidi wa kutegemea wa uharamu wa suala hilo, kwani utukufu wa viungo vya maiti haumzuilii alie hai kunufaika navyo.
Kwa kuzingatia kwamba jambo lililo muhimu zaidi hupewa kipaumbele kuliko jambo muhimu tu, na katika sheria ya Kiislamu inaruhusika kutenda lililokatazwa kwa dharura inayokubalika.
Ama endapo mtu hakuusia wala hakutoa ruhusa wakati wa uhai wake, basi ikiwa mawalii wake wataruhusu maiti hiyo itolewe kiungo fulani cha mwili wake inajuzu kufanya hivyo.
Endapo mawalii wake watakataa, baadhi ya wanazuoni wanasema haijuzu (Haifai) kutolewa kiungo hicho, na baadhi yao wanasema inakubalika, Lakini hapana shaka kuwa kufanya hivyo kwa kuokoa maisha ya mtu alie hai kunaruhusika (yaani inahalalika kutenda lililokatazwa, kwa kuzingatia kuwa kitendo cha kuhamisha kiungo cha mwanadamu hakifanyiki ila kwa dharura tu.
Iwapo mwenye kutolewa kiungo hicho yu hai, na kwamba hicho kiungo kitachotolewa kitapelekea yeye kupoteza uhai wake, (kwa mfano kuutoa moyo wake) itakuwa ni haramu kukitoa kiungo hicho, iwe ameruhusu au hakuruhusu kwani akitoa ruhusa hiyo itakuwa amejiangamiza nafsi yake.
Na kama hakutoa ruhusa hiyo, atakae tekeleza kitendo cha kumtoa kiungo na kupelekea mauti yake basi atakuwa ni mwenye kuuwa nafsi bila hatia bila ya haki, na yote hayo ni haramu kuyafanya.
Lakini endapo sehemu ya kiwiliwili chake itayotolewa haipelekei kupoteza maisha yake kwa maana ya kwamba ataweza kuishi bila kiungo hicho hapo kuna angalizo, kama wanavyosema wanazuoni.
Iwapo kutolewa kiungo kutamfanya asiweze kutekeleza mambo ya wajibu au itamsaidia kuingia katika kufanya mambo yaliyoharamishwa kwa mfano kukatwa mikono au miguu yote miwili ambapo atashindwa kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta maisha yake, basi katika hali hii ni haramu kutoa viungo hivyo iwe kwa kutoa idhini au kutokutoa idhini.
Na tukiacha hayo kama iwapo atatolewa figo zote mbili au macho au meno yote au akatolewa kiwango cha damu, basi iwapo katolewa bila ya ruhusa yake itakuwa ni haramu na itabidi alipwe fidia kama walivyo zungumza wanazuoni katika vitabu vya Fiqhi katika masuala ya kesi za jinai juu ya nafsi na viungo vya mwanadamu Lakini wanazuoni wengi wanaona kwamba hata akitolewa kwa idhini yake basi bado itakuwa ni haramu.
Na hoja yao inajengeka kutokana na utukufu wa mwanadamu ambao unakataa mtu kunufaika na viungo vya mwenzake, na kwamba kiungo kitachokatwa ni wajibu kukizika.
Imamu Annawawiy amesema katika kitabu Almaj muui J/3 Uk/149 Sherehe ya Muslim J/14 Uk/103 kuhusiana na uharamu wa kuunganisha nywele na nywele za binadamu : ( Na kwa kuwa ni haramu kutumia nywele za mwanadamu na viungo vyake vinginevyo kwa sababu ya utukufu wake basi zitazikwa nywele zake, kucha na viungo vyake vinginevyo.)
Lakini inawezekana kuirudi kauli hiyo kwamba kuunganisha nywele za mtu na mwengine ni suala ambalo wanazuoni wamekhtalifiana juu ya uharamu wake endapo halitafanyika kwa lengo la udanganyifu, na kughushi, na kwamba kuzika hizo nywele pia si wajibu kwani hakuna ushahidi ulio sahihi.
Amesema Ibnu Hajar katika kitabu chake cha Fathu Albari J12/Uk. 497 kwamba : Na katika hadithi ya Muawiya inajuzu kuunganisha nywele na sio wajibu kuzizika. Na dharura inaruhusu kutenda lililokatazwa.
Baadhi ya wale wanaoharamisha kukata viungo wametoa hoja ya kuwa mwili wa wa mtu sio mali yake kwa hivyo haijuzu kuutumia kwa hilo.
Lakini kauli hii haina ushahidi wowote, Mwanadamu hamiliki roho wala uhai wake kwa hivyo haijuzu kujiangamiza au kujiuwa isipokuwa tu kwa dharura ambayo ni jihadi na kuikinga nafsi katika maamuru ya Uislam.
Lakini viungo vya mwanadamu hivyo ni mali yake na anaweza kuvitumia iwapo hatopata madhara makubwa asiyoweza kuyahimili. Katika Uislamu hakuna kujidhuru wala kumdhuru mwenginewe.
Huu ndio muhtasari wa maudhui hii, kwamba hukumu ya kukiweka hai kiwiliwili au kukiuwa baada ya kuondoa kiungo Fulani ni jukumu la matabibu wahusika wanaoaminika.
Na pia iwepo dhana ya kweli au uhakika ya kuwa ambae ataingizwa kiungo hicho atanufaika nacho, vinginevyo itakuwa ni jambo la upuuzi na kupata lawama bila sababu.
Hilo ni kwa kuzingatia pia kuwa baadhi ya miili haikubali kuwekwa kiungo cha mtu mwengine ingawaje elimu na utafiti unajaribu kutaka kuhakikisha kuwa tatizo hilo linaondoka.
JEE INAKUBALIKA KUCHUKUA FIDIA KWA ANAETOA KIUNGO?
Iwapo tunakubali kuwa inajuzu kumtoa mtu kiungo cha mwili na kumpa mtu mwengine, jee inakubalika kuchukua (fidia) kitu chochote mkabala na kiungo hicho.
Baadhi ya wanazuoni wanaona kwamba haijuzu kufanya hivyo kwa ushahidi kuwa ni haramu kumuuza mtu alie huru awe mtu kamili au kiungo chake.
Hii ni kwa ushahidi wa hadithi ya Mtume (SAW) (Hadith Alkudsi ) amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu : Watu watatu mimi nitakuwa khasimu yao siku ya Kiyama na Yule ataenikhasimu basi na mimi nitamkhasimu , (Nao ni ) Mtu alietoa kwangu kisha akawacha, na mtu aliemuuza mtu alie huru na akala thamani yake na mtu aliemwajiri mfanyakazi akamkamilishia kazi yake kisha asimlipe ujira wake.
Baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba inajuzu kuchukua kitu mbadala kama vile malipo au hiba kama ambavyo mwanamke hulipwa kwa kumnyonyesha mtoto ziwa lake, na pia kwa kuwa hakuna dalili (ushahidi) wa kuharamisha.
Kwa hivyo vyovyote itavyokuwa ni bora kutozozana juu ya kiungo kilichotolewa, kwani kuokoa maisha ya mtu hakuhesabiwi sawa na malipo ya kitu chochote. Hata hivyo si vibaya kupokea kitu kama zawadi ambayo hutolewa tu kwa roho safi na bila ya shuruti iliyotajwa.
Katika kuzungumzia suala hili ni kwamba lilipokelewa suali katika Afisi ya Mufti Mkuu wa Nchi ya Misri juu ya kuchangia viungo vya mtu aliefariki kwa lengo la kuwasaidia wenye kuhitaji. Na tarehe 5 Disemba 1979 lilitoka jibu ( Angalia kitabu Alfatawa Al Islamiya J/10 Ukurasa wa 3702, na alikuwa Mufti ni Sh. Jad Alhaq Ali Jad Al haq ) ambapo alisema.
Na kila mtu anayo matakwa yanayo muhusu mwenyewe binafsi ingawa matakwa hayo yamefungika kwa kiwango chenye kufahamika katika aya ya 190 ya Sura ya Kwanza (Albaqarat) Mwenyezi Mungu amesema
(Na wala msijiingize kwa mikono yenu katika maangamizi na fanyeni yaliyo mema Hakika M.Mungu anawapenda waja wema ) Na katika aya 29 ya Surat Annisai ,amesema ( Na wala msiziuwe nafsi zenu hakika M.Mungu ni mpole kwenu).
Hilo pia linatuelekeza katika kauli za wanazuoni waliozungumzia Jihadi ya Nafsi na kuiiingiza nafsi katika kifo na kwa yale yaliyowajibishwa na Uislamu katika kumwokoa mtu anaeghariki, au anaeungua kwa moto kwamba inaweza kupelekea kuangamia kwa Mpigania jihadi au muokoaji.
Basi endapo daktari Muislamu mwenye uzoefu au asiekuwa Muislamu kama ilivyo katika Madhehebi ya Imamu Maliki (R.A) Kwamba atapochana sehemu ya mwili wa mtu alie hai kwa idhini yake na akatoa sehemu au kiungo chote kwa lengo la kumwingiza mtu mwengine alie hai kwa lengo la kumtibu, endapo itaonekana kwamba hakuna madhara kwa yule alietolewa kiungo (kwani madhara hayaondoshwi kwa madhara).
Na ikawa kile alichoingiziwa kitaleta faida basi kwa mujibu wa sheria ya Kiislam inajuzu, kwa sharti kuwa kisiwe kiungo kile kinachotolewa ni kwa ajili ya kukiuza au kuchukuwa kitu mbadala kwani kumuuza mtu au sehemu ya mtu muungwana ni kosa kisheria.
Mufti wa Misri ameendelea kwa kuzungumzia pia juu ya utukufu wa mwanadamu awe yuko hai au maiti katika kuhifadhi maisha yake hadi kumkafini na kumzika na pia kuharamishwa kufukua kaburi lake isipokuwa kwa dharura. Pia kukatazwa kuvunja mifupa yake akiwa hai au maiti.
Mwisho wa makala hii kwa mujibu wa fatwa iliyotangulia kuelezwa ni kwamba haijuzu kukata kiungo cha maiti kwa lengo la kukiingiza katika mwili wa mtu alie hai isipokuwa ni baada ya kuhakikisha kuwa mtu huyo amefariki dunia kwa uhakika . Na mauti kama yalivyoelezwa na wanazuoni katika vitabu vya Fiqhi (sheria ya kiislamu ) ni kuondoka kwa uhai katika kiwiliwili na alama zake ni kuparama kwa macho,miguu kukakamaa, kupinda kwa pua na kusita kabisa kwa moyo wake.
Katika msingi wa haya inajuzu kumtambua mtu kuwa ni maiti kwa vile alama za uhai zimemtoka kwa kudhihiri alama hizi tulizozitaja. Pia hakuna ubaya kutumia vifaa vya kitabibu ili kuhakikisha kuwa hata viungo vya hisia havina uhai.
Kwa kumalizia makala hii ni vyema nikanukuu vipengele vya maazimio yaliyopitishwa katika semina ya wanazuoni wa Fiqhi (Sheria ya Kiislam ) iliyofanyika mjini Amman mji mkuu wa Jordan tarehe 11 – 16 Octoba 1987 juu ya mashine za kusaidia kuweka uhai kwamba kuna alama mbili ambazo zikionekana itabainika kuwa mtu mwenye kuonekana hivyo ameshafariki.
Endapo moyo wake utasita kufanya kazi kwa ukamilifu na madaktari wakathibitisha kuwa kusita huko kwa moyo hakuwezi kuurejesha tena kufanya kazi yake.
Endapo viungo vyake vyote vya hisia pamoja na ubongo vimeharibika na wataalamu wa hayo wakahakikisha kuwa uharibifu huo hauwezi tena kuondoka na hakuna njia ya kuuondowa.
Katika hali hiyo endapo mtu amewekewa vifaa vya kumsaidia uhai, katika hali hii itabidi vifaa alivyowekewa viondolewe na kwamba imeshathibiti kwamba amefariki.
Hata hivyo, Mwenyezi Mungu ndie Mjuzi zaidi.