NA SHADYA MOHAMMED, OMWMA

WANANCHI wa shehia za Mtofaani, Hawaii na Mchikichini wameelezea kuwa wizi wa kutumia nguvu, udhalilishaji na matumizi ya dawa za kulevya ni miongoni mwa kero zinazowakabili kiasi cha kurudisha nyuma juhudi za maendeleo ya shehia zao.

Walieleza hayo katika mkutano uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi ambao ni miongoni mwa ziara ya Mkuu wa mkoa wa mjini magharibi idrissa kitwana Mustafa, uliofanyika katika uwanja wa Mazombi, shehia ya Hawaii, Unguja.

Walisema wananchi wanaotumia njia ya kutokea Misile Jeshini, hasa wanawake wamekuwa wakivamiwa na watu wasiojulikani na kuwapora vitu walivyonavyo huku wakiwatishia kwa mapanga.

“Katika kipindi cha sikukuu iliyomalizika juzi, hali hiyo  imejitokeza na kusababisha wanawake wawili kujeruhiwa kwa mapanga na kuwaibia simu zao, cha kushangaza vitendo hivyo hufanyiwa wanawake tu,” alisema Asha Mtumwa, mkaazi wa shehia ya Hawaii.

Aidha waliiomba serikali ya wilaya na mkoa kuliangalia kwa kina suala hilo kwa kuimarisha ulinzi katika  njia hiyo kwa vile inatumiwa na watu wengi wakiwemo wanafunzi wanapokwenda na kurudi skuli.

Aidha wananchi hao wameeleza kero nyengine kuwa ni kukosekana kwa skuli ya karibu na shehia hizo jambo linalosababisha watoto wao kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Walisema hali hiyo inachangia kushamiri kwa vitendo vya ushalilishaji na kuiomba serikali kuwajengea skuli kwa ajili ya watoto wao na kuzidisha kasi ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

“Tunapenda kuona hatua zikichukuliwa na adhabu kali zitolewe kwa wahusika wa vitendo vya ushalilishaji kwani vimeonekana kushamiri kwa kasi,” alieleza Rajab Idarous kutoka shehia ya Mtofaani.