KAMPALA, UGANDA

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amewataka Waafrika kutumia lugha ya kiswahili ili kuwa na umoja barani humo.

Akizungumza katika siku ya Muungano wa Afrika ya upatanishi inayolenga kutathimini mafanikio ya muungano wa Waafrika, Museveni amesema kiswahili ni lugha ambayo haiegemei upande wowote kiasi kwamba inaweza kuunganisha, tafauti na lugha nyengine za kikabila.

Katika akitoa hotuba hiyo, Museveni pia alisema anasikitishwa na kukosekana kwa mshikamano wa Waafrika.

Kupitia ujumbe wake wa mtandao wa Twitter, rais huyo wa Uganda aliandika

“Waafrika tayari wana mambo mengi ya kufanana au kuhusiana, hakuna sababu ya sisi kutoungana, ni rahisi kwa Waafrika kuungana kuliko watu wa Ulaya, lakini la kushangaza hatuendi kwenye mwelekeo huo’’.

Aidha Museveni aliendelea kusema kuwa, “wakati wazungu wanapoamua kukutana, wanaanza kujiuliza tunafaa kuongea lugha gani? Kiitalia? Kiingereza?, Kiholanzi?, kijerumani? Lakini katika Afrika tunaweza kutumia lugha ya kiswahili isiyoegemea upande wowote kutuunganisha , si ya kabila lolote, sio ya mtu yeyote’’. Alisisitiza