NA HAFSA GOLO
MBUNGE wa Jimbo la Donge, Dk. Khalid Salum Mohamed, amewataka wajasiriamali kutumia vyema maonesho ya sabasaba kwa kubadilishana uzoefu sambamba na kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na ubora na viwango vinavyostahiki.
Waziri Khalid ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ,Sera na Uratibu wa Baraza la Wawakilishi aliyasema hayo wakati alipokuwa akiwaaga kikundi cha wajasiriamali wanawake wa jimbo la Donge kinachoelekea nchini Tanzania Bara katika maonyesho ya saba saba.
Aliwafahamisha kwamba maonesho ya aina hiyo yana umuhimu katika kuinua biashara ,kupata soko la kuuza biadhaa wanazozalisha,kubadilishana uzoefu miongoni mwa wajasiriamali sambamba na kujenga mtandao wa pamoja.
“Hakikisheni safari yenu ni moja ya fursa muhimu ya kuongeza kipato na kuongeza ujuzi katika uwajibikaji wa majukumu yenu ya kila siku”,alisema.
Alisema katika maonesho hayo lazima wawe wabunifu katika kusarifu bidhaa wanazozizalisha, ili ziweze kupata soko zaidi la ndani na nje ya nchi na la utalii kwani limekuwa sana kutokana na mpango wa serikali wa kukuza sekta hiyo.
Pamoja na hayo Dk.Khalid aliwafahamisha wajasiriamali hao kwamba maonesho kama hayo yatawasaidia wao na wajasiariamali wengine wa Zanzibar kuwajengea uwezo wa kushiriki katika maonesho mengine makubwa yanayofanyika katika nchi mbali mbali jambo la msingi ni kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na sifa na ubora ambao utawavutia wateja mbali mbali .
Hata hivyo, alisema ,serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wajasiriamali wote nchini wanaweza kutumia fursa sambamba na kuwajengea mazingira wezeshi ya kupata mitaji kupitia mfuko wa uwezeshaji wananchi.