Ang’oa wakurugenzi

 Watendaji wasimamishwa

 Ni kwa kushindwa kuwajibika

 Wengine awapa uangalizi zaidi

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasimamisha kazi wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya za Unguja na baadhi ya wakurugenzi wa taasisi na idara nyengine serikalini.

Dk. Mwinyi alitoa agizo hilo jana wakati alipofanya mkutano wa majumuisho uliofanyika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakili, baada ya kukamilisha ziara yake katika Mikoa mitatu ya Unguja.

Akizungumza na viongozi na watendaji Dk. Mwinyi alisema amewasimamisha kazi wakurugenzi, watendaji na wafanyakazi kwa kuhusika na vitendo vya wizi, kutowajibika katika dhamana zao na ubadhirifu wa mali za serikali.

Aliwataja waliohusika na kadhia hiyo kuwa ni pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya Mjini, Magharibi ‘A’ na ‘B’, Kaskazini A na B, Kusini, wilaya Kati na mkurugenzi wa SMIDA.

Akizungumzia ziara aliyofanya katika mikoa mitatu ya Unguja, Dk. Mwinyi aliwataka watendaji kubadilika kwa kigezo cha kuwepo changamoto mbali mbali hususan katika sekta za kijamii na utoaji huduma, huku baadhi ya changamoto hizo zikisababishwa na ukosefu wa fedha na nyingine zikitokana na utendaji usioridhisha.

Alisema kumekuwa na mikataba mingi ya kifisadi katika baadhi ya halmashauri za wilaya akatoa mfano wa halmashauri ya wilaya Mjini inayoingia mikataba ya aina hiyo na kampuni za simu na kuingia mikataba katika uwekaji wa mabango.

Alisema kumekuwepo ukusanyaji mdogo wa mapato katika halmashauri ya wilaya Mjini, kiasi cha wilaya hiyo kufanana na halmashauri zilizoko vijijini.

Alieleza hali mbaya inayoikabili sekta ya afya nchini na kusema haridhishwi na utendaji kazi wa wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, kwa kukosa miundombinu bora, kutokuwa na vitendea kazi, kushindwa kutoa huduma muhimu na hivyo wananchi kukosa huduma sahihi.

Aliiagiza wizara hiyo kuwa na mipango maalum ya kupata fedha pamoja na kuzitumia vizuri fedha hizo, huku akibainisha wizara hiyo kuwa na vyanzo mbali mbali vya kuingiza mapato.

Alisema kwa muda mrefu sasa Serikali imekuja na wazo la kuwa na mpango wa Bima ya Afya, lakini kwa kipindi chote hicho hakuna kitu kilichofanyika.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwasimamisha kazi Wakurugenzi wa Idara ya Tiba, Idara ya Kinga pamoja na Idara ya Rasilimali watu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha, akaiagiza Taasisi ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) pamoja na Jeshi la Polisi kuchunguza suala la wizi wa fedha za Shirika la Umeme (ZECO) katika vituo vya kununulia umeme na kutaka hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika na kadhia hiyo.

Sambamba na hilo, Dk.  Mwinyi akaagiza kusimamishwa kazi wafanyakazi waliohusika na ung’oaji wa nguzo za umeme katika eneo la Mwachealale.

Rais Dk. Mwinyi aliikumbusha ZECO wajibu wake wa kupeleka nguzo za umeme pamoja na Transfoma katika shughuli za kuwaungia umeme wananchi, “ZECO wajibu wa kupeleka nguzo za umeme na Transfoma ubaki kwenu, … suala la ada nalo liitazamwe upya”, alisema.

Akigusia sekta ya ujasiriamali, Dk. Mwinyi aliagiza Mifuko yote ya Uwekezaji iliopo nchini iunganishwe (ukiwemo Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mfuko wa Walemavu, Vijana, SMIDA n.k), kwa vile haijafanya kazi ipasavyo, kwani fedha zimekuwa zikitolewa ovyo na bila hesabu, pamoja na kutokuwepo marejesho.

Aidha, akaitaka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuwawezesha wajasiriamali, huku akitaka fedha zitumike vizuri, na akatoa mfano wa matumizi mabaya ya fedha kwa SMIDA, ambao katika kipindi cha mwaka mzima iliwawezesha wananchi 27 pekee kutoka mtaji wa shilingi bilioni mbili.

Akizungumzia suala la usafi katika jiji la Zanzibar, na kusema ni eneo la barabara ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kuelekea hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja pekee, ndio inayosafishwa kwa vile yeye amekuwa akitumia kuelekea Ikulu.

Alisema asilimia 90 ya fedha za Mradi wa (ZUSP) ambazo ni dola milioni 90, zimetengwa kwa ajili ya kupendezesha Mji, lakini hakuna matunzo ya miti iliyopandwa, mbali na fedha nyingi kutumika kwa ajili ya kuilipa Kampuni ya Usafi

Alisema serikali inakusudia kuja na mradi maalum wa kupendezesha Mji kwa kuwa na barabara zenye lami, maeneo ya waenda kwa miguu pamoja na mambo mbali mbali, huku jukumu la kusimamia usafi likiwa chini ya usimamizi wa Manispaa.

Kuhusiana na sekta ya ardhi na makaazi, Dk. Mwinyi alieleza kuwepo migogoro mbali mbali katika maeneo aliyoyatembelea, na kusema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi imejikita katika utauzi wa migogoro, badala ya kuja na mipango mipya ya maendeleo.

Dk. Mwinyi aliahidi kuunda Tume itakayokuwa na wajibu wa kupitia migogoro yote ya Ardhi na hivyo Wizara kubakia na jukumu la kuendeleza makaazi mapya kwa wananchi.

Alisema watendaji wote watakaobainika kuhusika au kuwa chanzo cha migogoro hiyo, Tume itakayoundwa itawachukuliwa hatua.

Aidha, akazungumzia sekta za udhalilishaji wa kijinsia pamoja na upatikanaji wa Dawa za Kulevya na kuzitupia lawama Mamlaka zinazohusika kwa kutokuchukua hatua zozote za msingi  katika kukabiliana na jambo hilo.

Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau kushirikiana kuondoa udhalilishaji nchini, sambamba na kuagiza Watuhumiwa wote wa makosa hayo kuwekwa ndani.

Alisema vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na watoto unaanzia kwenye jamii (skuli, madrasa), hivyo akaitaka jamii kuondokana na muhali.

Akigusia Dawa za Kulevya, alisema mihadarati hiyo imekuwa ikiingia nchini kupitia njia za Bandari na Uwanja wa Ndege na kubainisha uwepo wa baadhi ya watendaji wanaoshirikiana na wahalifu kupitisha dawa hizo na kuleta athari kubwa kwa vijana, ambapo wengi wao hujiingiza katika vitendo vya wizi.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuiagiza ZAECA kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watendaji wote waliohusika na Tenda ya Vifaa ‘dhaifu’, kwani mazingira yanaonyesha kuwepo viashiria vya rushwa katika kadhia hiyo.

Aliutaka Uongozi wa ZAWA kusimamia kwa umakini mkubwa maendeleo ya Mradi wa maji wa Exim Bank ambao utawanufaisha wananchi wa Wilaya za Magharibi ‘A’ na ‘B’ pamoja Wilaya ya Kati na kuwataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha Mkandarasi anakamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.