MNAMO Julai 3 na Julai 4 mwaka huu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alifanya ziara kukagua miradi ya maendeleo na miradi ya kijamii katika mkoa wa Kusini Unguja.

Siku kwanza katika ziara hiyo ya siku mbili, alianzia wilaya Kusini na siku iliyofuata alihitimisha ziara yake kwa kutembelea miradi ya maendeleo na ya kijamii wilaya ya Kati.

Katika ziara hiyo maeneo mengi ambayo Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuyatembelea alikumbana na vilio vya wananchi kukosa huduma muhimu za msingi za jamii kama maji, umeme, barabara nakadhalika.

Inasikitisha sana kuwaona wananchi wakilalamika mbele ya rais wakitaka huduma muhimu za kijamii, lakini ukitazama unaona wananchi hawana jinsi ni bora wamlalamikie rais kwa sababu yeye anajua na kuumwa zaidi na shida zao.

Kwa tunavyoelewa malalamiko ya wananchi mbele ya rais ya kukosa huduma za msingi yana maana nyingi, kwanza watendaji dhama wameshindwa kutekeleza majukumu yao, pili watendaji wameshindwa kutekeleza agizo la rais linalowataka kuwa wawabunifu, tatu watendaji wanaendelea kufanyakazi kwa mazoea.

Tunasema hivyo kwa sababu malalamiko mengine yaliyowasilishwa na wananchi mbele ya rais katika ziara ya Mkoa wa Kusini Unguja, hayahitaji fedha bali yanahitaji mbinu, maarifa na matumizi kidogo ya akili za kiongozi mwenye mamlaka na hatimaye kuyapatia ufumbuzi.

Huwa tunajiuliza masuali mengi watendaji wako wapi hadi wananchi wawasilishe kero zao kwa rais? Kila siku wanapokwenda kazini katika taasisi zao wafanafanyakazi gani? Je rais alipokuwa hajafanya ziara changamoto za wananchi hazikuwepo?

Majibu ya masuali hayo maana yake ni kwamba baadhi ya viongozi waliopewa dhamana hawajayajua maeneo yao ya kiutendaji na hili tunakumbuka lilikuwa moja ya agizo la rais alililowapa watendaji na viongozi wa serikali.

Ilipoingia madarakani awamu ya nane wananchi walikuwa na matumaini makubwa kwamba serikali inakwenda kuzipatia ufumbuzi changamoto za msingi, ingawaje hadi sasa matumaini hayo bado wanaendelea kuwa nayo.