HATIMAYE Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekamilisha ziara ya kuitembelea mikoa na wilaya zote za Zanzibar aliyoianza Julai 3 mwaka huu.

Ziara hiyo ilianzia mkoa wa Kusini Unguja, kwa kuzitembelea wilaya za Kusini na wilaya ya Kati na baadae akaelekea mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuzitembelea wilaya za Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’.

Mwishowe alimalizia ziara hiyo katika mkoa wa Mjini Magharib na mnamo Julai 7 mwaka huu katika ukumbi wa Idrisa Abdulwakil uliopo Kikwajuni alifanya majumuisho ya ujumla ya ziara yake hiyo.

Katika mkutano huo wa majumuisho Dk. Mwinyi alibainisha maeneo 10 ambayo kimsingi ndiyo changamoto kubwa alizozibaini wakati walipotembelea maeneo mbalimbali kwenye ziara hiyo.

Kwa muktadha wa udogo wa nafasi ya tahariri hii ni vigumu kuchambaua maeneo hayo yote 10 kwa undani, lakini kikubwa kilichobainika ni kwamba viongozi wengi waliopewa dhamana katika taasisi wameshindwa kuwajibika.

Katika maeneo hayo vilio vya wananchi ni pamoja na kukosa maji ya safi, kutofikiwa na huduma za umeme, skuli, barabara, wajasiriamali kushindwa kuwezeshwa nakadhalika.

Kasi ya utendaji kwa viongozi wateule waliopewa dhamana katika taasisi mbalimbali serikalini ni ndogo mno na kiukweli hawajakidhi matarajio makubwa waliyonayo wananchi kwa serikali yao.

Kwa mfano tunajiuliza, hivi kweli chungu ya changamoto zilizoibuliwa na wananchi katika maeneo mbalimbali ambayo rais alifanya ziara wateule ngazi ya ukurugenzi walikuwa hawazielewi?

Kama wateule walikuwa hawaelewei uwepo changamoto ambazo wananchi walizibainisha katika zaira ya rais, inaonesha wazi kwamba wameshindwa hata kufuata maagizo 13 aliyoyatoa wakati alipowaapisha mawaziri.

Inamaa na wateule hawazielewi kwa undani taasisi zao, hawaelewei huduma wanazopaswa kuzitoa kwa wananchi kwa niaba ya serikali na hii inathibitisha wanafanyakazi kwa mazoea.

Tunahisi Dk. Mwinyi anastahiki kutekeleza maamuzi anayoyachukua ya kuwawajibisha watendaji walioshindwa kutekeleza vyema majukumu yao, kwa mfano kweli mpaka leo tunahimizana kuhusu usafi?

Wakurugenzi wa halmashuri za wilaya na manispaa baada ya fedha kuzielekeza kwenye miradi ya maendeleo ambayo itakwenda kubadilisha maisha ya wananchi mamilioni ya fedha yanatumika katika uendeshaji ikiwemo malipo ya maposho.

Hatua za kuwaondoa wakurugenzi walioshindwa kutekeleza na kusimamia majukumu yao, bila shaka itakuwa fundisho kwa wengine katika kuhakikisha wanawajibika na kuendana na kasi ya awamu ya nane.

Wakati mwengine kijipu kidogo usipokitafutia matibabu kitakuwa ndio sababu ya kukwata mguu, hivyo wale wachache lazima tuwaweke pembeni ili safari iendelee kwa wanaweza kusababisha matatizo makubwa mbele ya safari.

Tunapopewa nafasi za kiuongozi tuhakikishe tunawajibika na kutekeleza vyema majukumu yetu, sio kujifaharisha kwa ma-prado na viti vya kunesanesa maofisini tukidhani nafasi hizo tumepewa kama fadhila.

Tunadhani ziara hiyo iwazindue wateule kwenye nafasi zao, kwanza waujue muelekeo, waujue mtazamo na matajio ya rais na serikali ya awamu ya nane, haipendezi na inasikitisha sana kila rais anapokwenda anasema sijaridhishwa.

Uongozi ni dhamana tuwajibike, tusimamie waliochini yetu, tuwaelekeze na kuwafahamisha na pia tuwasikilize kwa sababu waliochini nao wanamawazo yanayoweza kutufanya tusonge mbele.