NAIROBI, KENYA

BENKI Kuu ya Kenya (CBK) imeziorodhesha kauti za Nairobi, Mombasa na Kiambu kuwa ni kaunti tajiri zaidi nchini Kenya kulingana na matawi ya benki.

Utafiti wa CBK kama ilivyoripotiwa na gazeti la Business Daily, ulitambua kwamba nusu ya matawi ya mabenki yaliyopo nchini yanapatikana katika kaunti hizo ikionesha kipato kikubwa kinachopatikana katika kauti hizo ikilinganishwa na nyengine.

Kwa mujibu wa utafiti huo wa CBK, Nairobi, Mombasa na Kiambu zina jumla ya matawi 794 ya benki ambayo ni sawa na asilimia 53 kwa benki zote ilizopo nchini Kenya ambazo ni 1,502.

Nairobi ndio inaongoza kuwa na idadi kubwa ya benki ambapo ina jumla ya asilimia 39.5, ambapo pamoja na serikali kubuni serikali ya ugatuzi ili kugawana utajiri, Nairobi bado inatawala kaunti nyengine.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kaunti hizo tatu nchini Kenya za Nairobi, Mombasa na Kiambu zinamiliki utajiri wa asilimia 30.9 katika taifa hilo.

Kaunti 20 kati ya 47 zina chini ya matawi 10 ya benki. Samburu, Tana River na Mandera zina benki chache pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu kuliko Mombasa.

Kaunti za Mlima Kenya miongoni mwa gatuzi tajiri Mnamo Agosti 2020, utafiti wa Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) uliorodhesha kaunti za Mlima Kenya miongoni mwa gatuzi tajiri nchini.

Meru, Nyeri, na Kirinyaga ziliorodheshwa ya pili, tatu na nne mtawalia na utafit huo ulionyesha wakazi wana uwezo wa kujilisha. Katika kaunti ya Meru, 18% ya wakazi walitajwa kama maskini kati ya idadi ya watu 1, 455, 848.