Akiri kazi ya urais ina ugumu wake

Aanika mambo muhimu ya kuyaendeleza katika kazi yake

NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

“NIWAAMBIE bila ya kupepesa kwamba kazi ya Rais ni ngumu, lakini kwa vile tunafanya kazi kama Taasisi na ina vyombo kadhaa vinavyosaidia kutekeleza jukumu hili”.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwajibu wahariri na wandishi wa habari wakati alipofanya mazungumzo nayo jana, Ikulu Dar es salaam, ikiwa ni siku 100 za kushika madaraka ya Urais wa Tanzania Machi 19 mwaka huu.

Alisema urais unapofanya kazi kama Taasisi, hapo ndio huwa urahisi wake, kwamba Rais hafanyikazi pekee yake, lakini kama unavyojuwa serikali ina sekta kadhaa, ambapo kila linalojitokeza kuna sekta yake ya kulishughulikia.

Rais hupelekewa kwa ajili ya kutoa maelekezo au maamuzi, ambapo anapopelekewa huwa tayari limeshashakatwa, sambamba ndani ya Ofisi ya Rais kuna wasaidizi kadhaa ambao wanamsaidia kuzishakata na kumpelekea kwa kutoa maamuzi.

“Niseme kwamba sio rahisi kihivyo kuna ugumu wake kwa sababu unatakiwa kujua kila kitu kinachotokea ndani ya nchi yako na kinapokuja kisiwe kigeni kwako, usome utafute, kwa siku moja ‘file’ zinaingia 30 hadi 25 ndani ya Ofisi ya Rais na uzifanyie kazi zote kwa kutoa maelekezo au kuzishusha kwa wasaidizi kwa ajili ya kukusaidia”, alisema.

Alisema  kwa hiyo kazi ya Urais ni ngumu na ngumu zaidi unapokuwa kwamba hukujitaarisha kuichukua, ambapo pale unapojitaarisha ukajaza fomu, ukalipa, ukapiga kampeni unakuwa umeshajipanga kwenda kugombea nafasi hiyo.

“Lakini kwa upande wangu nilizungumka ndio, nilipiga kampeni, nikawashawishi watu tuchaguweni nikijua kwamba nina bonge la kaka juu yangu atabeba mimi nitakuwa namsaidia, lakini kwa mapenzi ya Mungu limetokea lililotokea ule mzigo sasa umekuja mabegani kwangu”, alisema.

Alisema hakupata uzito mkubwa sana wa kuupokea kwa vile anajua kilichomo, ambapo alikuwa anajua wameahidi nini kwa wananchi, kwa kujua wamejipangaje, kuwatumikia wananchi lakini kulifanya kama yeye lina ugumu wake.

Hata hivyo aliwathibitishia kwamba analiweza kwenda nalo jukumu la urais wa Tanzania, pamoja na kuwa na usaidizi wa taasisi zote na wandishi wa habari, hivyo anajua atafika kwa pamoja kwa vile sio kazi yake peke yake bali ni yetu sote.

Alieleza katika siku 100 alizokaa katika madaraka, hata yeye alikuwa anasikiliza katika vyombo vya habari kwa kila sekta inasema yaliyofanyika, mpaka anashangaa kwamba na hayo yamefanyika kwa kweli ilikuwa ni habari hata kwake.

HALI YA UCHUMI

Akigusia hali ya uchumi alisema wameweza kuhimili vishindo vya kuteremka kwa uchumi wa dunia kutokana na janga la COVID -19, ambapo Tanzania imeweza kulihimili kwa thamani ya pesa yetu bado ipo sawa haijashuka, mfumuko wa bei upo vizuri na wanahakiba ya kutosha ya fedha za kigeni inayoweza kuwachukuwa hata miezi sita bila ya kukusanya nyengine.

Rais Samia ‘Tunahakiba ya miezi sita mbele na kiasi hicho kidunia kinakubalika na ndivyo kati ya vigezo vilivyotupandisha katika uchumi wa kati, kwa sasa tunahakiba ya Dola za Marekani Bilioni 4.97 ambayo inatuchukuwa kwa miezi sita’, alifafanua.

Lakini mfumuko wa bei bado umebakia asilimia 3.3 hivyo upo vizuri, ambapo aliwahakikishia watanzania kuwa miradi mikubwa iliyoanzishwa ikiwemo Bwawa la kufufua umeme na mradi wa reli ya kisasa inaendelea kwenda vizuri na ujenzi wake.

Bajeti iliyopitishwa hivi karibuni wamepanga fedha nyingi katika kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo umeme vijijini, maji, barabara za vijijini pamoja na kuwa na mipango ya kuweza kupata fedha ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.

HALI YA VYOMBO VYA HABARI

Alisema atashirikiana na kufanya kazi kwa karibu zaidi na vyombo vya habari na changamoto zinazowahasibu, zitafanyiwa kazi kwa karibu na kushirikiana na wadau wa tasnia hiyo.

Rais Samia alisema vyombo vya habari baadhi yao vinafungwa kutokana kushindwa kujiendesha kwa madai vimenyimwa matangazo, jambo ambalo hajalikuta katika meza yake na wala hakuna ‘file’ hilo.

Matangazo yapo ya serikali na yale yanayotolewa na sekta binafsi, ambapo zaidi kinachohitajika hapo ni ushindani wa vyombo hivyo na uwepesi wa kuweza kuingia katika ushindani wa kupata matangazo ili iwasaidie kuendesha vyombo vyao.

“Wakati wa uongozi wa huu sitozuia matangazo ya serikali kuja katika vyombo binafsi, kwani ni kinyang’anyiro na uwezo wa mtu wa kupata matangazo”, alisema.

Pia kulikuwa kuna suala la kulipa madeni ambalo Waziri Mkuu ameshalishughulikia, hivyo na yeye atalifanyiakazi kwa kushirikiana na Waziri Mkuu ili kuona jinsi watavyoweza kulipa kidogo kidogo, lakini katika madeni hayo lazima kufanyike tathmini na kuweza kuthibitisha.

SHERIA YA HABARI

Alisema ipo haja ya kuangaliwa sheria ya vyombo vya habari, ili kuona changamoto zilizopo ziweze kufanyiwa kazi.

“Katika kuyafanya hayo hatutoyafanya sisi serikali pekee yao watashirikiana na jukwaa la wahariri na taasisi nyengine za vyombo vya habari ili wakae pamoja na kuziangalia kwa maslahi ya taifa letu.

Baraza la Habari (Jukwaa la Habari) aliwajibu kuhusiana na kupatiwa ruzuku ya serikali, alisema Bunge na Mahakama, kati ya mihimili mitatu ya Dola (serikali) hivyo lazima ipate ruzuku kutoka serikalini lakini kwa Jukwaa hilo wataendelea na mazungumzo.

Alisema Jukwaa la Habari bado halijawa lakini alihimiza kuendelea mazungumzo ili waone watafika wapi katika kufanya kazi pamoja na kama ipo ruzuku waone jinsi gani inaweza kutoka, hivyo waendelee na mazungumzo kwa vile siku zote hupatikana kwa ufumbuzi.

Sekta ya Habari, vyombo vya habari ni moja tunavyofanya kazi, hivyo hatuwezi kupanga mipango mikubwa bila ya kuangalia sekta hiyo, kwa kuwepo katika miradi mbali mbali ya maendeleo na dira ya maendeleo kwa vile ni wadau wakubwa na serikali.

Rais Samia alisema kuhusiana na magazeti yaliyofungiwa, yafunguliwe kwa mujibu wa sheria na wameshamaliza adhabu zao, hivyo aliwashauri waende wakaombe leseni upya lakini hadi sasa bado hawajafanya hivyo.

“Kama wapo waliomaliza adhabu zao waende waombe leseni upya, lakini alisisitiza kuwa sheria za nchi lazima zifuatwe, licha ya sheria lakini kuna ile heshima na adabu za kiafrika huwezi kusimamia na gazeti lako kumchambua mtu na kuna mwengine siyo mengine ndio wakati na wewe unajua unamama, unadada na familia”, alisema Rais Samia.

Alieleza kuwa wanahabari wana uwezo wa kuikosoa serikali lakini waonyeshe na njia, kwa hiyo lazima iwepo heshima wataenda pamoja na watafika.

JANGA LA CORONA

Akizungumzia kuhusiana na janga la corona, Rais Samia alisema wakati anaingia katika madaraka alitamani alishughulikie kama linavyoshughulikiwa ulimwenguni, hivyo alitaka kujua ukubwa wa tatizo hilo kwa Tanzania.

Aliunda kamati ya kitaalamu na kuwapa wiki tatu na wakenda kufanya na kuleta ripoti ya kwanza na kuwapa tena kazi na kuwaambia wakajipange kitaaluma hasa katika suala zima la chanjo kama dunia inavyotaka na zipi zinazohitajika na jinsi ya kuzihifadhi.

Sambamba na hilo, lakini alisema aliangilia watu wanaofanya kazi katika mashirika ya kimataifa wanaotoka nje lakini wapo Tanzania (international community) kama wa China wanaoishi hapa, ambao waliomba kuwaruhusu chanjo zao ziletwe na kuweza kuchanjwa.

Pia aliwaambia wataalamu hao wakajipange hususani katika suala la kiuchumi kuwa fedha za mapambano ya maradhi hayo zitapatikanaje, ambayo kazi hiyo aliwapa ndani ya wiki tatu hadi mwezi mmoja.

Alisema juzi Baraza la Mawaziri walikaa na kujadili yale waliyoletewa na maamuzi yalifanyika waende kama Dunia inavyokwenda katika vita hivyo vya COVID-19.

Wimbi la kwanza Tanzania ilipata athari ya CORONA lakini haikuwa kwa kiasi kikubwa  kwa sababu ilichukuliwa tahadhari zote, ambapo wimbi la pili ilipiga limeathiri nchi kidogo kuliko la kwanza.

Rais Samia alisema hivi sasa wimbi la tatu limeanza katika ulimwengu, ambapo alisisitiza wapo wagonjwa katika wimbi hili,  hadi taarifa za juzi zinasema takwimu kuwa kuna wagonjwa wa zaidi ya 100 kati yao chini ya wagonjwa 70 wapo katika matibabu ya gesi na wengine wanatibiwa kawaida.

Alitoa wito kwa watanzania waendele kujikinga ili hiyo idadi isiongezeke, kwa kuwasikiliza washauri na watalaamu wa afya kwa kunawa maji yanayotiririka na kuvaa barakoa.

Akigusia suala la chanjo alisema wameamua kwenda kama ulimwengu unavyokwenda wachanje kwa hiari, kwa watanzania anayetaka atachanja asiyetaka basi.

“Wameamua kwa sababu ya watanzania wengi ambao ni wafanyabiashara wameshakwenda kuchanja nje ya nchi wapo waliochanja Dubai, Afrika Kusini, huko wanapokwenda na wapo hapa wanaendelea na shughuli zao”, alisema.

“International Community’, wameamua kuwaruhusu kuleta chanjo zao kwa kushirikiana Wizara ya Afya na watalaamu wa ndani ziletwe na kupokea ili wachanje chini ya usimamizi wa wataalamu wao na watanzania”, aliongeza.

Aidha alisema chanjo hiyo lazima uchanjwe mara mbili, hivyo lazima watasimamiwa tena kuna kuchanjwa mara ya pili, ambapo kwa Tanzania wameamua kuingia katika wimbi la kuchanjwa mwaka 2022 ambao mwisho ilikuwa Juni 15, mwaka huu, hivyo kama hukusema ulimwenguni wangepata chanjo ya mwaka 2023.

Tanzania iliharakisha na kusema wao wamo katika chanjo ya CORONA, hivyo wataalamu wanaifanyia kazi chanjo ipi ije nchini, kwa ajili ya kuchanjwa wananchi, ambapo mashirika mengi ya nje yamejitokeza kusaidia lakini bado watalaamu wanaendelea kulifanyia uchambuzi.

“Kazi ya kupambana na CORONA sio ya serikali pekee yake, lakini pia wananchi kwa ujumla wao wajitahidi kuchukua hadhari zile zile walizokuwa wanachukuwa kama kupiga nyungu zitwasaidia sawa, lakini za wataalamu kukosa mikono, vaa barakoa na epukeni mikusanyiko”, alisema Rais Samia.

Alisema hali ni mbaya nchi zinaendelea kupigwa na hata majirani zetu wapo vibaya juu ya maradhi hayo, ambapo mipakani tayari kumeanza kupokewa kwa taarifa hizo za ugonjwa, hivyo  kingeni sana watoto.

“Serikali ipo vizuri na mashirika mengi yamejitokeza kusaidia na hivi sasa kuna fedha kama Dola za Marekani milioni 470 za kupambana na magonjwa hayo ikiwemo kuagiza vifaa, chanjo na pia kusaidia zile sekta zilizoathiriwa na jangwa hilo”, alisema mama Samia.

Akizungumzia suala la kuwepo ‘package’ au fungu maalum kwa vyombo vya habari, juu ya magonjwa hayo alisema ni zito kwa vile hata serikali uchumi wake umeshuka kutoka asimilia 7 hadi kufikia asilimia nne, ambapo kwa mwaka huu wanaomaliza umeweza kupanda hadi kufikia asilimia 5.5.

Kwa sasa hatutoweza kwa sababu hata uchumi wenyewe wa nchi unahitaji kutafuta “package”,

KILIMO NA UTARATIBU WA MASOKO

Alisema Tanzania ipo vizuri katika masoko, kwa vile kinachozalishwa nchini Rwanda wanakula, Kenya, Uganda, Sudani, Burundi na Comoro ndio wote wanakula bidhaa za hapa.

Kilichokuwa kinakwamisha ni masuala ya usafiri na usafirishaji, akitolea mfano nchi ya Jamhuri ya DRC- Congo, Tanzania wanachozalisha leo kinaweza chote kikaliwa na kumaliza lakini usafirishaji ndio unakwamisha, hivyo lazima kujengwa kwa barabara, reli za kisasa, meli katika maziwa ili kuweza kusafirisha mazao kwa nchi za jirani, ambapo kwa soko SADC na Afrika Mashariki lipo.

MIKUTANO YA SIASA NA KATIBA MPYA

Rais Samia Suluhu Hassan alisema wakati anafungua Bunge alisisitiza kuwa atakaa na wenzake wanasiasa ili kuona wanakwendaje katika suala la siasa nchini.

“Hivi sasa Tanzania inachangamoto nyingi kuna janga la COVID-19, na uchumi umeshuka hivyo kuna mambo mengi ya kushughulikia kwa sasa katika nchi”.

Alisema “Nakwenda kuifungua nchi, kwa sababu uchumi umeshuka hivyo anataka kupandisha uchumi, hivyo ikifunguliwa nchi kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kazi ambayo imefanya vizuri.

Wawekezaji waliosajiliwa kipindi hiki cha mwezi Machi mpaka Mei mwaka huu ni mara mbili na wale waliosajiliwa mwaka jana kipindi kama hicho.

Alisema wawekezaji wengi wanakuja Tanzania sasa, ambapo wanapofungua hivyo, uwekezaji uwe mkubwa, ajira ipatikane pesa izunguke mifukoni kwa wananchi kipato na uchumi wa mtu mmoja mmoja ukuwe na kuendelea kukusanya mapato.

Alieleza tutanuwe wigo wa mapato yetu ya kukuza maendeleo, hilo linataka nchi iwe na amani na utulivu na nchi iwe imesimama vizuri, hivyo katika kufanikisha hilo ni jukumu la kila mmoja wetu ndani ya nchi anajukumu hilo serikali, vyombo vya habari, wanasiasa na kila mmoja anajukumu hilo.

Alisema uchumi wa Tanzania ukipanda kila mmoja atafaidika na uwekezaji ukipanda ajira utapatikana na uchumi utazunguka na mifuko yetu itakuwa mizuri.

“Tukafanye kazi, tujenge taifa la watanzania wote sio la mmoja mmoja, tukafanyeni kazi, alisisitiza.