MNAMO Julai 7 mwaka huu dunia ilipa mshituko pale vyombo vya habari vilipotoa taarifa za kuuawa kwa aliyekuwa rais wa Haiti, Jovenel Moïse ambapo taarifa zilieleza kuwa alipigwa risasi akiwa katika nyumba ya makaazi yake.

Katika shambulizi hilo ambalo lilisababisha rais huyo kupoteza uhai, washambuliaji walimgeukia mkewe naye walimshambulia na kumuachilia majeraha na hivyo kuwahishwa hospitali.

Mjane huyo aliswafirishwa hadi Miami nchini Marekani kwenda kupata matibabu ya majeraha yaliyotekelezwa na mamluki waliomuua mumewe, ambapo hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii alikakariwa akielezea kile kilichotokea siku aliyouawa mumewe.

Martine alisema mauaji yalifanyika baada ya wahalifu kupenya kuingia ndani usiku, ambapo mara baada ya kuingia katika makaazi ya rais kwa haraka sana walitekeleza shambulizi.

“Ghafla, mamluki waliingia nyumbani kwangu na kumuua mume wangu kwa risasi,” bi Moïse alisema katika rekodi hiyo, akielezea wakati ambapo washambuliaji walimuua mumewe.

“Kitendo hiki hakina jina kwa sababu lazima uwe mhalifu sugu kumuua rais kama Jovenel Moïse, bila hata kumpa nafasi ya kusema neno moja,” aliongeza.

Alidai kamba mumewe alikuwa akilengwa kwa sababu za kisiasa, hasa akitaja kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba ambayo ingeongeza nguvu zaidi za rais. Watu hao ambao hawajulikani alisema, “wanataka kuua ndoto ya rais”.

“Ninalia, ni kweli, lakini hatuwezi kuiacha nchi ipotee,” aliongeza. “Hatuwezi kuruhusu damu ya rais Jovenel Moïse, mume wangu, rais wetu ambaye tunampenda sana na ambaye alitupenda sisi, kupotea bure”.

Moïse, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa rais wa Haiti, taifa maskini zaidi katika Amerika, tangu 2017, ambapo utawala wake ulikuwa mgumu kwani alikabiliwa na tuhuma za ufisadi na kulikuwa na maandamano mengi ya kumpinga.

Uchaguzi wa bunge ulipaswa kufanywa Oktoba mkwa 2019 lakini mizozo imechelewesha kufanyika kwa uchaguzi huo, hivyo Moïse aliendelea kutawala chini ya amri ya rais, ambapo alipanga kufanya kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba ya nchi hiyo mnamo mwezi Septemba mwaka huu.

Mnamo mwezi Februari mwaka huu, wapinzani walipasa sauti wakimataka aondoke ofisini, ambapo Moïse alisema jaribio la kumuua na kupindua serikali lilishindwa.

Nani amehusika na mauaji ya rais wa Haiti? Polisi nchini humo imesema imemkamata raia wa nchi hiyo aliyetumia ndege binafsi kushirikiana na watu wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji ya rais Jovenel Moise.

Mkuu wa Polisi wa Haiti, Leon Charles alimtambulisha mtuhumiwa huyo ni Christian Emmanuel Sanon, mwenye umri wa miaka 63 anayeishi Florida, Marekani.

Mkuu huyo alisema mtu huyo alikwenda Haiti kwa kutumia ndege binafsi mwanzoni mwa mwezi Juni akiwa na walinzi binafsi na alitaka kuchukua nafasi ya urais.

Mkuu huyo wa polisi hakueleza nia ya Sanon, zaidi ya kusema zilikuwa za kisiasa na kwamba aliwasiliana na mtuhumiwa mmoja baada ya kukamatwa.

Charles aliwaambia waandishi habari kwamba nia ya washambuliaji hao awali ilikuwa kuhakikisha usalama wa Sanon, lakini baadae lengo lilibadilishwa na walimpa mmoja wa wauaji hati ya kumkamata rais na kwamba maofisa wa polisi walipata vitu kadhaa kwenye nyumba ya Sanon.

Ndani ya nyumba ya Christian Emmanuel Sanon, zilipatikana kofia yenye nembo ya mamlaka ya kupambana na biashara haramu ya dawa za nchini Marekani, DEA.

Alikuwa na masanduku sita ya kuwekea bunduki, maboksi 20 yenye risasi, vibao vinne vyenye namba za magari zilizosajiliwa kwa namba za Jamhuri ya Dominika, magari mawili na mawasiliano aliyofanya na watu wasiojulikana.

Charles alisema jumla ya raia 26 wa Colombia wanatuhumiwa kumuua rais Moise Jumatano iliyopita, ambapo 18 kati yao wamekamatwa pamoja na raia wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani.

Mkuu huyo wa polisi alibainisha kuwa kinachoendelea ni kuwasaka watuhumiwa watano wa uhalifu huo ambao anaamini bado wamo nchini Haiti hawajatoka nje ya nchi hiyo.

Mkuu huyo wa polisi wa Haiti alisema wanashirikiana na maofisa wa ngazi ya juu wa Colombia kubaini taarifa zaidi za wanaotuhumiwa kupanga mauaji hayo, na kuangalia lini waliondoka Colombia na nani alilipia tiketi zao.

Wanaotuhumiwa wa mauaji ya rais huyo waliwaeleza wapelelezi kwamba walitaka kumkamata kiongozi huyo na sio kumuua, ambapo hayo yamebainika katika ripoti iliyotolewa na gazeti la Marekani la Miami Herald.

Gazeti hilo liliwanukuu watu waliozungumza na watuhumiwa 19 wanaoshikiliwa hadi sasa, gazeti hilo limeeleza kuwa lengo lao lilikuwa kumkamata Moise na kumpeleka kwenye ikulu ya rais.

Duru za karibu na intelijensia zimesema watuhumiwa wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani, James Solages na Joseph Vincent wamewaambia wapelelezi kwamba walikuwa wakalimani wa kitengo cha makamandoo wa Colombia ambacho kilikuwa na hati ya kumkamata Moise.

Miami Herald, limesema raia wa Colombia wanaoshikiliwa wamesema walitumwa kufanya kazi Haiti na kampuni ya ulinzi ya CTU yenye makao yake Miami, inayoendeshwa na muhamiaji wa Venezuela, Antonio Emmanuel Intriago Valera.

Wananchi wa Haiti katika maeneo ya mji mkuu Porto-Au-Prince wamepanga kuandamana wiki hii kupinga mauaji ya Moise na kumpinga waziri mkuu wa mpito na anayeiongoza nchi kwa sasa, Claude Joseph.