NA ZAINAB ATUPAE
MCHEZO wa ligi daraja la pili mkoa wa Mjini Magharibi hatua ya nne bora kati ya New City na Kundemba FC uliochezwa juzi ulishindwa kukamilika kwa wakati kufuatia New City kugoma kuendelea na mchezo huo.
Hali hiyo ilitokea baada ya Kundemba kuandika bao la pili mnamo dakika ya 75 kupitia kwa Omar Yussuf na kulalamikiwa na wachezaji wa City wakipinga maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo kukubali bao hilo.
Baada ya kusubiri kwa muda, mchezo huo ulivunjwa na uongozi wa chama cha soka mkoani humo (UWERFA) uliupa ushindi Kundemba ambayo ilipachika bao lake la kwanza katika dakika ya 23 lililofungwa na Ali Makame.
New City yenye mastakimu yake katika shehia ya Dole wilaya ya Magharibi ‘A’, ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Juma Said kwenye dakika ya 34 na kuufanya mchezo huo kwenda mapunziko timu hizo zikiwa nguvu sawa.
Kwa matokeo ya mchezo huo uliotimua vumbi uwanja wa Mao Zedong ‘B’ saa 1:00 asubuhi, Kundemba ilifikisha pointi nne huku New City ikibakiwa na pointi tatu timu hizo zikibakiwa na mchezo mmoja mmoja ili kumaliza ligi hiyo ndani msimu huu na kupatikana bingwa ambae atapanda daraja.