NA MWAJUMA JUMA
WADAU wa soka visiwani Zanzibar wameombwa kuisaidia timu ya soka ya Wanawake ya New Generation, ambayo inajiandaa kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati, itakayofanyika nchini Kenya kuanzia Julai 17 mwaka huu.
Ombi hilo limetolewa na mmiliki wa timu hiyo Farid Mohammed Hamza, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi huko katika uwanja wa mazoezi ya Wazee uliopo Maisara mjini Zanzibar.
Alisema wamekua katika maandalizi mazuri ya kujiandaa na michuano hiyo, lakini wanahitaji kusaidiwa kutoka kwa wadau wengine ili kuwa mazuri zaidi.
Alisema mpaka hatua ambayo wamefikia wamepata msaada mkubwa kutoka kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tabia Maulid Mwita, ambae amekua mstari wa mbele na asilimia 80 ya safari hiyo.
Alisema waziri huyo amekua akifanya vikao na kuwaita kila mara na kusaidiwa kwa baadhi ya vifaa ambavyo wanafanyia mazoezi.
Pamoja na waziri huyo pia alisema na uongozi wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) nao umekuwa ukiwapatia taarifa za mara mara juu ya yale yanayotokea.
Alifahamisha kwamba haya ni mashindano makubwa ambayo maandalizi yake yanataka muda mrefu, lakini kutokana na uharaka wake wamekuwa wakilazimisha baadhi ya mambo ili kufanikisha.
Timu hiyo inafanya mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo katika uwanja wa Wazee Maisara asubuhi na jioni na inatarajia kuondoka nchini Julai 15.