BAADA ya miongo miwili ya vita vilivyoitwa vya kupamabana na ugaidi nchini Afghanistan Marekani iliyoongoza vita hivyo na washirika wake wameondosha majeshi yao nchini humo.

Marekani na washirika hao walikuwa kipambana na makundi yaliyokuwa yakiendesha harakati za kigaidi ya Taliban na Al Qaeda, ambapo hivi sasa rasmi nchi hiyo inajitegemea kwa ulinzi baada ya wanajeshi wa kigeni kuondoka.

Kambi ya mwisho ya wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan ni ile iliyokuwakitovu cha uendeshaji wa operesheni za kijeshi za angani ya Bagram ambapo wanajeshi wa kigeni tayari wameondoka katika kambi hiyo.

Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani viliingia nchini humo Disemba mwaka 2001 na kambi ya Bagram ilitengenezwa kuwa kituo kikubwa chenye uwezo wa kuchukua hadi wanajeshi 10,000.

Rais Joe Biden alitangaza kuviondoa vikosi vyote vya Marekani kufikia Septemba 11 mwaka huu, lakini wakati Marekani ikiviondoa, kuna ripoti kwamba wanamgambo wa Taliban wameanza upya operesheni zao za kigaidi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo, wataliban wanaendelea na uvamizi wa maeneo mbalimbali ya Taliban na hiyo ni kudhihirishwa kuwa vita vya viaka 20 ilivyoongozwa na Marekani na washirika wake nchini humo havikufanikiwa kuingoa mizizi ya ugaidi.

Hivi sasa serikali ya Afghanistan imepeleka mamia ya makomando na wapiganaji katika kukabiliana na mashambulizi ya kasi yanayofanywa na wanamgambo wa Taliban katika upande wa kaskazini wa nchi hiyo.

Ripoti zinaeleza mapigano yamepamba moto katika mikoa kadhaa ya Aghanistan, lakini waasi wameelekeza zaidi kampeni yao kali katika eneo la kaskazini mwa nchi, ambako wamekamata wilaya kadhaa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Mamia ya wanajeshi na wapiganaji wanaoiunga mkono serikali wamepelekwa katika mikoa ya kaskazini ya Takhar na Badakshan ambako wataliban wamekamata maeneo makubwa, bila mapigano yoyote.

Maofisa wa ulinzi wa Afghanistan wamesema wanakusudia kuzingatia zaidi katika kuilinda miji mikubwa, barabara na miji ya mipakani kutokana na mashambulizi ya Taliban.

Waziri wa ulinzi wa Afghanistan, Bismillah Mohammadi alisema vikosi vya serikali viko katika hali nzito ya kijeshi, na kuongeza kuwa mapambano na wapiganaji wa kundi la Taliban yameshika kasi.

Mohammadi alitoa uhakikisho kwamba vikosi vya taifa kwa kushirikiana na vikosi vya ndani vinavyoiunga mkono serikali, vitatumia rasilimali na uwezo wake wote kuilinda nchi na watu wake.

Hivi karibuni zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Kiafghanistan walikimbilia nchi jirani Tajikistan hatua ambayo imeilazimu nchi hiyo jirani kuimarisha ulinzi kwenye mpaka huo kwa kuwapeleka wanajeshi wake, ambapo wanajeshi hao waliingia nchini humo kukimbia mashambulizi ya Taliban.

Rais wa Tajikistan, Emomali Rakhmon ameamuru kupelekwa wanajeshi 20,000 wa akiba ili kuongeza ulinzi katika mpaka kati ya nchi yake na Afghanistan, ambapo kuna taarifa kuwa askari hao wa Afghanistan tayari wamesharejea nchini mwao.

Namna ambavyo wataliban wameingia kwa nguvu kubwa za kijeshi kuyakamata maeneo makubwa ya Takhar na Badakhshan ni pigo kubwa la kisaikolojia kwa serikali ya Afghanistan.

Mikoa hiyo miwili kwa wakati mmoja ilitumika kama ngome za muungano wa kijeshi uliopambana na Taliban katika upande wa kaskazini wakati wa vita vikali vya miaka ya 1990 na haikuwahi kukamatwa na wanamgambo wa itikadi kali.

Huku Taliban ikijiimarisha kijeshi dhidi ya vikosi vya serikali, rais wa Marekani Joe Biden ametetea uamuzi wa kuviondoa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, akisema Waafghanistan wanastahili kuamua mustakabali wao na hatotuma wanajeshi nchini humo.

Akizungumza katika ikulu ya White House, hivi karibuni, Biden alisema jeshi la Afghanistan lina uwezo wa kutosha wa kupambana na wanamgambo wa Taliban.

Aidha rais huyo alikanusha ripoti kwamba idara ya ujasusi Marekani inatazamia kwamba serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na Marekani itaanguka katika kipindi cha miezi sita ijayo tu huku kukiwa na tahadhari kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini humo.

Rais huyo alisema wanajeshi wote wa Marekani isipokuwa 650 watakaoulinda ubalozi wa Marekani mjini Kabul, watakuwa wameondoka kufikia Agosti 31, huku maelfu ya wakalimani wa Afghanistan watapelekwa katika maeneo salama.

Biden alikiri baada ya miaka 20 ya vita nchini Afghanistan, majeshi ya Marekani kuuangusha utawala wa Taliban kufuatia yale mashambulizi ya Septemba 11, uwezekano wa serikali ya Afghanistan kuweza kuitawala nchi yote ni mdogo mno.

Kulingana na Biden, Marekani imeondoa wanajeshi wake baada ya kutimiza malengo yake katika nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kummaliza Osama bin Laden, kulidhoofisha kundi la kigaidi la Al-Qaeda na kupunguza mashambulizi Marekani.

“Mwaka 2014 walisema tuendelee kukaa kwa mwaka mmoja zaidi, kwa hiyo tukaendelea kupigana na wanajeshi wetu wakaendelea kufa, mwaka 2015, ikawa vivyo hivyo”, alisema.

Rais huyo alibainisha kuwa kwa takriban miaka 20 ya uzoefu nchini Afghanistan imeonesha na hali inathibitisha kuwa mwaka mmoja zaidi wa mapigano Afghanistan si suluhisho ila mwanzo wa kusalia huko kwa kipindi kisichobainika.

Biden alisema ana imani na majeshi ya Afghanistan ambayo kwa miaka sasa yamekuwa yakipewa mafunzo na kupokea silaha kutoka kwa Marekani kwa ajili ya kupambana na Taliban.

Rais huyo wa Marekani aliziomba nchi zote katika ukanda huo kusaidia kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kati ya pande zinazozozana huku akiitaka serikali ya Afghanistan kutafuta muafaka na Taliban kwa ajili ya amani ya nchi yao.

Marekani na washirika wake, ilichukua hatua za kuivamia Afghanistan kijeshi mara tu baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001, shambulio maarufu lilifanyika dhidi ya Marekani na kuua karibu watu 3,000.

Katika shambulizi hilo ndege zilizotekwa zilielekezwa kwenye jengo la World Trade Center mjini New York, Pentagon katika jimbo la Arlington, Virginia na ndege ya nne iliangushwa katika kiwanja kimoja huko Pennsylvania.

Osama Bin Laden, aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, baade alitambuliwa kuhusika na shambulio hilo.

Taliban, kundi la kijihadi lililoendesha Afghanistan na kumlinda Bin Laden, lilikataa kutoa ushirikiano. Kwa hivyo, mwezi mmoja baada ya shambulio la 9/11, Marekani ilifanya mashambulio ya angani dhidi ya Afghanistan kulikabili kundi hilo.