NAIROBI, KENYA

OFISA mmoja wa polisi ambaye amekuwa mafichoni baada ya kuwaua watu wawili amepatikana akiwa ameaga dunia.

Mwili wa Caroline Kagongo ambaye amekuwa akisakwa baada ya kuwaua watu wawili, umepatikana nyumbani kwa wazazi wake kaunti ya Elgeyo Marakwet eneo la Rift Valley.

Kulingana na polisi ofisa huyo alimpiga risasi mwenzake John Ogweno Julai mwaka huu, na kisha kutorokea eneo la Juja viungani mwa mji wa Nairobi alipomuua mwanamme mwingine aliyetambuliwa kama Peter Ndwiga kwa kumpiga risasi katika chumba cha malazi hotelini.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimemnukuu Kamishna wa Kanda ya Rift Valley George Natembeya kuthibitisha kisa hicho.

Ripoti hizo zinasema Kagongo alijiua kwa kujipiga risasi kutumia bastola ambayo alikuwa amejihami nayo na anayoshukiwa kuitumia kutekeleza muaji ya hapo awali.