KAMPALA, UGANDA
POLISI nchini Uganda, imesema kuwa imemtia nguvuni mtuhumiwa wa pili kwenye jaribio la mauaji ya waziri wa kazi na ujenzi nchini humo Edward Katumba Wamala.
Kenye taarifa waliyoitoa kwa waandishi wa habari jijini Kampala, polisi walisema mtuhumiwa huyo waliyemtia nguvuni anatambulika kwa jina la Huzaifa Wampa (30), ambaye zamani alikuwa kiongozi wa umoja wa bodaboda.
Polisi walitoa picha na mtuhumiwa huyo mbele ya waandishi wa habari ambapo ataungana mtumiwa wenziwe Walusimbi Kamada, ambaye aliwahi kuwa ofisa katika jeshi la Uganda.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Huzaifa Wampa alitiwa mikononi na polisi akiwa kwenye maficho katika kijiji cha Kikomeko kilichopo wilaya ya Luwero iliyopo katikati ya Uganda.
“Tumemkamata mtuhumiwa wa pili wa jaribio la mauaji ya waziri tumekutana kijijini akiwa amejificha tumepekua katika makaazi yake na tumebaini baadhi ya vitu alivyotumia siku ya shambulizi hilo akiwemo pikipiki yenye trangu nyekundi na namba za usajili UEO 375D”, alisema msemaji wa polisi, Fred Enanga.
Msemaji huyo wa polisi alisema kuwa baada ya mahojiano na Wampa alikiri kuhusika kwenye matukio kadhaa ya mauaji kwenye maeneo mbalimbali nchini humo pamoja na ujambazi.
Fred Enanga alisema kinachofuata hivi sasa ni kumuunganisha kwenye kesi ya mauaji, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kuhakikisha inawatia nguvuni washukiwa wote.
Mnamo Juni 1 mwaka huu, watu wenye bunduki wakiwa kwenye pikipiki walilishambulia gari la waziri wa kazi na usafirishaji Edward Katumba Wamala, ambapo katika shambulizi hilo mtoto wa waziri Brenda Nantogo na dereva wake Haruna Kayondo waliuawa.