NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano imetenga shilingi bilioni moja na milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam cha taasisi ya Sayansi za Bahari (TSB) kilichopo Buyu, Zanzibar.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekolojia, Prof. Joyce Lazaro Ndalichako alitoa kauli hiyo mara baada ya kufanya ziara ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa miradi ya elimu ya juu nchini Tanzania na itasaidia kupunguza changamoto ya masafa kwa wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho kutembea umbali mkubwa.

Aliwahakikishia kwamba serikali haiwezi kuwekeza na kuona fedha zinapotea hivyo aliahidi kwamba watafanya mapitio ya miradi yao ili kuona jengo hilo linapatiwa fedha na linakamilika na kuweza kutoa vijana ambao watasaidia katika maendeleo ya nchi yao.

“Tutaanza kujenga mwaka huu wa fedha ili kuona madhumuni ya kuanzishwa taasisi hii yanafikiwa kama ilivyokusudiwa na bajeti ya mwakani tutahakikisha zinatengwa kwa ajili ya kumaliza jengo hili”, alisema.

Prof. Ndalichako alibainisha kuwa taasisi hiyo ni muhimu katika uchumi wa nchi kwani Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anasisitiza kutoa elimu yenye ujuzi wa moja kwa moja.

Hata hivyo, alibainisha kuwa wanapitia tena mitaala yao ili kuona ujuzi unawafikia vijana na kuona vijana hawawachwi nyuma katika kujenga uchumi wa nchi yao.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa chuo hicho Dk. Margareth Kyewalyanga, alisema taasisi hiyo tafiti zao zimejikita kuchangia uchumi wa buluu hasa katika nyanja za uvuvi na ufugaji wa viumbe wa majini kama samaki wa aina mbalimbali chaza wa lulu majongoo bahari, kaa na mwani.

Hata hivyo alisema wanafanya tafiti katika utunzaji na utumiaji endelevu wa rasilimali mbalimbali za bahari ikiwemo mikoko, matumbawe, majani bahari, wanyama watambaao vimelea na vielea vitumiavyo kulisha mbegu za samaki

Akizungumzia changamoto zinazowakabili alisema ni pamoja na kukosekana kwa vyumba vya mihadhara vya kutosha, chumba cha mikutano, maabara za wanafunzi wa shahada ya awali hali ambayo inasababisha wanafunzi kurundikana wakati wa masomo ya vitendo, utumiaji na ufundishaji wa tehama bado unakwamisha na kutokiwepo kwa maabara maalum ya kompyuta ambayo nayo ilipangwa kujengwa katika eneo ambalo bado halijaanza ujenzi wake.

Naye mbunge wa jimbo la Kiembesamaki, Mohammed Maulid Ally alisema chuo hicho wanakitegemea sana hasa kwa wakati huu nchi inakwenda katika uchumi wa bluuu hivyo aliwataka vijana kuitumia fursa hiyo katika kusoma Ili waweze kufikia malengo ambayo serikali inayataka.

Nao wanafunzi wa chuo hicho waliipongeza serikali kwa hatua hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa itaweza kuwaondolea changamoto ambayo ilikuwa wakiililia muda mrefu.