NA  NIZAR VISRAM

KWA muda wa siku 11 mnamo Mei mwaka huu ulimwengu ulishuhudia makombora ya Israel yakiporomoshwa katika ukanda wa Gaza nchini Palestina.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), matokeo yake watu 278 waliuawa, wakiwemo watoto 66, wanawake 39 na wakongwe 17. Watu 9,000 walijeruhiwa, nyumba 17,000 ziliteketezwa na watu zaidi ya 90,000 wakakosa mahali pa kuishi.

Israel ililenga na kuboma zahanati takriban 30, hospitali saba na kliniki 11. Pia iliteketeza kituo cha Covid 19 na kumuua mkurugenzi wake. Ikateketeza vituo viwili vya magari ya kubebea wagonjwa pamoja na zahanati ya kina mama na watoto.

Viwanda vinavyoajiri watu 1,500 vilipigwa makombora na kusababisha hasara ya dola milioni 20 hadi 25. Moto ulipokuwa ukiwaka wazima moto waliitwa. Lakini walipofika nao wakapigwa makombora na kwa hivyo moto ukazidi kuenea.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inasema Gaza yenye wakazi milioni mbili ikawa eneo lisilokalika na hali yake ikawa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya mashambulizi ya Israel.

Katika mashambulizi hayo Israel ilitumia ndege za kivita kiasi cha 80. Ni pamoja na ndege za kisasa ziitwazo F-35s ambazo Israel ilipewa na Marekani. Ndege hizo zilitumika Gaza kama majaribio ili marubani wake wapate uzoefu wa kuzitumia katika vita. Uzoefu huo uliwasaidia pia watengenezaji wake, Lockheed Martin, nchini Marekani wakisaidiwa na Italia.   

Hivi ndivyo Israel ilivyoishambulia Gaza ikidai kuwa eti inajilinda. Hoja hii ilikataliwa ulimwenguni kwa sababu siku hizi kila kitu kinajulikana na kuonekana kupitia mtandao wa kimataifa. Ndipo wadadisi huwa wanauliza maswali kem kem na Israel inaumbuka.

Wasemaji wa Israel wanapobanwa hujaribu kujibu kwa kuuliza “Je, kama nchi yenu ingeshambuliwa nanyi mgefanya nini?” Mwanahabari mmoja makini alijibu “Nchi yetu haijaishambulia na kuikalia Palestina kimabavu.”

Halafu Israel inapoulizwa kuhusu watoto wa Kipalestina wanaouawa, hudai kuwa eti  “Ni Hamas ndio wanaotulazimisha tuwauwe”.

Hoja hizo hazifui dafu mbele ya ukweli, ndipo Israel huja na hoja nyingine kuwa wanaoilaumu Israel wana chuki dhidi ya Wayahudi. Yaani eti ukiilaumu au kuikosoa sera na vitendo vya Israel maana yake unawachukia Wayahudi (anti-Semitism).

Hizi ni mbinu na propaganda zinazotumiwa na Israel wakati wa kujibu lawama zinazowaelemea kote duniani. Katika lugha ya Kihibrania (Kiyahudi) mbinu hizo huitwa “Hasbara.” Ni mbinu za upotoshaji na upindishaji ukweli.

Kwa mfano, msemaji wa kijeshi wa Israel, luteni kanali Conricus alitangaza kuwa jeshi lake linakusudia kutumia vifaru ili kuishambulia Gaza. Baadae ikagundulika kuwa hiyo ilikuwa mbinu ya kuwafanya wapiganaji wa Hamas kujitokeza hadharani ili waweze kupigwa kirahisi.  Conricus alipoulizwa akajibu eti hilo lilikuwa “kosa” yaani eti “walighafilika”.

Mbinu nyingine waliyotumia ni kusambaza video ikionyesha eti Hamas wanarusha maroketi yao kutoka majengo wanamoishi raia. Ikagundulika kuwa video hiyo ni feki kwa sababu ilitangazwa kutoka Syria tangu Disemba 2019.

Mbinu kama hizi zilijulikana ulimwenguni kote, kwani picha za mauaji ya Israel huko Gaza  zilisambaa kote duniani. Si ajabu kwa hivyo ulimwenguni Israel ililaaniwa na Wapalestina wakaungwa mkono.

Kuna mifano mingi. Ni vizuri tukaangalia michache. Maelfu ya wananchi walimiminika katika miji ya Livorno na Milan nchini Italia, London, Birmingham na Liverpool nchini Uingereza, Adelaide na Sydney nchini Australia, Frankfurt na Berlin nchini Ujerumani na Paris nchini Ufaransa. Katika jiji la London peke yake wananchi takriban 180,000 waliandamana.

Na nchini Marekani maelfu walikusanyika jijini Washington wakiilani serikali yao kwa kuisaidia Israel. Walitaka Israel iwekewe vikwazo na serikali ya Marekani iunge mkono mahakama ya kimataifa (ICC) ili iweze kuihukumu Israel kwa uharamia wa kivita. Mikutano na maandamano kama hayo yalifanyika pia barani Afrika katika nchi za Morocco, Tunisia, Kenya na Afrika Kusini.

Na katika bandari ya Oakland nchini Marekani wafanyakazi waligoma kuihudumia meli ya Israel na matokeo yake ikalazimika kutia nanga wiki mbili baharini.

Hali kadhalika katika bandari za Livorno na Genoa nchini Italia wafanyakazi walikataa kupakia meli iliyokuwa inataka kusafirisha silaha kuelekea Israel.  Pia katika bandari ya Durban nchini Afrika Kusini wafanyakazi walikataa kupakua meli ya Israel.

Walichukua hatua hizi kutokana na uamuzi wa umoja wa wafanyakazi wa bandari kote duniani kuzigomea meli za Israel. Ni uamuzi wa kimataifa kutokana na maombi ya muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Palestina.

Katika jiji la Leicester nchini Uingereza wanaharakati wa chama cha mshikamano na Palestina walivamia kiwanda kinachotengeneza ndege zisizo na rubani (drone) kwa niaba ya Israel.

Walifunga milango wakisema nia yao ni kuzuia Uingereza kuipa Israel silaha zinazotumika kuwaua wananchi wa Gaza. Hatua kama hizo zilichukuliwa pia katika bandari ya Runcorn nchini Uingereza ambako wanaharakati walivamia kiwanda kinachotengeneza drone kwa ajili ya Israel.

Zaidi ya wanamuziki 600 wa kimataifa waliandika risala ya kuwaunga mkono Wapalestina, na kuwataka wanasanaa wenzao duniani kukataa kutembelea na kufanya maonyesho nchini Israel.

Wakati huohuo wabunge nchini Ireland walipitisha azimio la kulaani uvamizi wa Palestina uliofanywa na Israel. Hii ni mara ya kwanza kwa bunge barani Ulaya kuchukua msimamo kama huu. Na chama cha Sinn Fein nchini humo imeiandikia barua serikali ya Ireland kuitaka imfukuze nchini humo balozi wa Israel. Barua hiyo imesainiwa na wananchi zaidi ya 88,000.

Aidha, maaskofu wa Jamhuri ya Ireland wamelipongeza bunge lao kwa kupitisha azimio la kuunga mkono Wapalestina. Wameitaka serikali yao kuitambua dola ya Palestina kama alivyofanya Papa mwaka 2013.

Nayo halmashauri ya jiji la Belfast (Ireland Kaskazini) imepitisha azimio la kuzitaka serikali za Ireland na Uingereza kumfukuza balozi wa Israel. Azimio lilisema uhusiano wa kibalozi na Israel haukubaliki kutokana na sera zake ya kikaburu na uhalifu wa haki za binadamu

Bunge la jimbo la mji mkuu wa Brussels imepitisha azimio la kuilaani Israel kwa kuivamia Palestina. Azimio hilo limeitaka serikali kuiwekea Israel vikwazo vya kiuchumi na kibiashara na kuitambua Palestina kama dola.

Na huko Australia wanahabari zaidi ya 720 walisaini barua wakilalamika jinsi vyombo vyao vya habari vinavyotangaza kwa upendeleo vita baina ya Israel na Hamas. Kutokana na barua hiyo, waandishi kadha walionywa na mashirika yao ya utangazaji wafute majina yao la sivyo wangefukuzwa kazi.

Halikadhalika nchini Canada wanahabari walilalamika kuhusu jinsi suala la Palestina linavyoripotiwa. Wakaandika risala wakisema wao wamekuwa wakiambiwa na mabozi wao wasitumie neno Palestina.

Risala hiyo ikasainiwa na watu zaidi ya 2,000 na ikasambazwa katika vyumba vya habari. Matokeo yake baadhi ya walioandika risala wakazuiliwa wasiandike habari za Palestina na Israel

Nao watu mashuhuri wapatao 682 duniani kote waliandika barua ya wazi kwa rais Joe Biden wa Marekani, wakimwambia aikanye Israel iache kuwagandamiza na kuwadhalilisha Wapalestina.

Waandishi wa barua hiyo ni pamoja na mshindi wa zawadi ya Nobel Tawakkol Karman kutoka Yemen, mwanazuoni wa Israel Profesa Ilan Pappe, mwanazuoni wa Marekani Profesa Noam Chomsky, mwanasheria  mkuu mstaafu wa Israel, spika mstaafu wa bunge la Israel, rais mstaafu wa Ireland, Bi Mary Robinson na wabunge wa Uingereza

Nchini Marekani katika jiji la Seattle umoja wa waalimu (SEA) ulipitisha azimio la kuwaunga mkono Wapalestina na kutaka Israel  iwekewe vikwazo (BDS). Wakaitaka idara ya polisi Seattle iache kushirikiana na majeshi ya Israel.

Mwanaharakati mmoja wa chama hicho Emma Klein alisema: “Mimi nikiwa mwalimu wa Kiyahudi nina faghari kushirikiana na wenzangu wa SEA. Uamuzi uliochukuliwa ni sahihi kwa vile unapinga udhalimu wa Israel” .

Baada ya mashambulizi ya siku 11 ikatangazwa kuwa Israel na Hamas zimefikia “makubaliano ya kuacha vita.” Lugha hii inayotumika ni ya kupotosha, kwani Israel inaendelea kuikalia Palestina, pamoja na kupora makazi ya Wapalestina na kupanua makazi ya walowezi  haramu.

Katika hali kama hii ni dhahiri kuwa Wapalestina watatumia kila njia halali ya kujikomboa kutoka ukoloni huu wa Kizayuni. Hiyo ni haki yao chini ya sheria ya kimataifa. Ndio maana mratibu wa Umoja wa Mataifa(UN) kuhusu amani katika mashariki ya kati, Bw Tor Wennesland, alionya kuwa usitishwaji huu wa mapigano  “siyo imara”.

Amesema kweli, kwani huu sio usitishwaji wa kwanza wa mapigano baina ya Israel na Wapalestina . Profesa Michael Lynk, mchunguzi wa UN kuhusu haki za binadamu nchini Palestina, amesema:“ Ni bahati mbaya kuwa katika maeneo ya Gaza, Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi  vurugu na vita vimekuwepo kwa muda mrefu –  miaka ya 2018, 2014, 2012, 2008-09, 2000, 1987 na kadhalika. Hii ni sehemu ya historia ya Palestina iliyovamiwa.”

Na ndipo leo hii tunaona maelfu ya walowezi kutoka Israel wakiandamana katika mitaa ya Jerusalem huku wakipeperusha bendera ya Israel na kuimba “Waarabu wauliwe” na “Nakba ya pili inakuja.” Nakba (maafa kwa Kiarabu) ni tukio la 1948 wakati Wapalestina takriban 800,000 walipotimuliwa kwa mtutu wa bunduki kutoka ardhi ya Palestina ambayo leo inaitwa Israel. Uchochezi kama huu ni jambo la kawaida kwani hata serikali inayotawala Israel inaongozwa na waziri mkuu ambaye aliwahi kusema “Maishani mwangu nimewahi kuwaua waarabu, nami sioni tatizo lolote kwa hilo.”

Kuhusu mashambulizi ya Israel katika Gaza, gazeti la New York Times nchini Marekani limesema Israel imetenda uharamia wa kivita. Wataalamu wameliambia jarida hilo kuwa Israel ililenga makombora huko Gaza bila ya kutoa taarifa kwa raia wasio na hatia na bila ya kuwa na habari kuhusu wanacholenga.

Walisema ingawa Israel ilidai kuwa walikuwa wakiwalenga Hamas, lakini hawakuwa na ushahidi wowote kuwa katika majengo waliyobomoa walikuwemo wapiganaji wa Hamas.

Hivi ndivyo walivyouawa raia katika ukanda wa Gaza. Mwandishi nguli nchini Israel, Gideon Levy amesema propaganda za Israel (hasbara)  hazimdanganyi mtu yeyote – labda inajidanganya Israel yenyewe. Levy akamnukuu aliyekuwa balozi wa Israel, hayati  Yohanan Meroz, ambaye aliwahi kusema:

“Sisi Waisraeli tutapiga mayowe ya “ugaidi”. Tutalalamika kuwa Wayahudi tunabaguliwa na tutakumbusha jinsi tulivyouawa nchini Ujerumani. Tutadai Israel ni nchi yetu tuliyoahidiwa. Yote haya ni propaganda na haitatusaidia, kwani ulimwengu unaelewa fika jinsi tunavyowatendea Wapalestina”

 nizar1941@gmail.com