PORT-AU-PRINCE, HAITI
WAZIRI mkuu wa Haiti, Claude Joseph amethibitisha kuuawa kwa rais wa nchi hiyo, Jovenel Moise katika shambulio lililofanyika katika makaazi yake mjini Port-au-Prince.
Katika taarifa rasmi aliyoitoa baada ya shambulizi hilo, Joseph alisema makaazi ya rais huko Port-au-Prince yalishambuliwa na watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha majira ya saa 7 usiku za nchi hiyo.
Joseph alisema rais huyo aliuawa akiwa nyumbani kwake na wapiganaji wanaodaiwa walikuwa wakizungumza lugha ya kingereza na kihispania.
Taarifa zinasema mke wa Moise, alijeruhiwa katika shambulio hilo na anaendelea kupata matibabu, waziri mkuu Joseph, akiwataka wananchi kuwa watulivu wakati huu waliohusika wakisakwa na polisi.
Jovenel Moïse mwenye umri wa miaka 53, amekuwa madarakani tangu mwezi Februari mwaka 2017, baada ya mtangulizi wake, Michel Martelly kung’atuka mamlakani.
Wakati wa Moïse ofisini ulikuwa mgumu kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi na alikabiliwa na mawimbi ya maandamano ya mara kwa mara ya kupinga serikali.
Mwaka wa 2019 wakati wa moja wapo ya maandamano kama hayo rais huyo alisema hatoondoka madarakani kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa magenge yaliyojihami na walanguzi wa dawa za kulevya.
Upinzani nchini humo ulisema kwamba kipindi cha miaka mitano ya Moïse kilipaswa kumalizika Februari 7 mwaka huu, lakini tangu muda huo amekuwa madarakani.