SANTO DOMINGO, HAITI

MKUU wa Baaraza la Seneti la Haiti, Joseph Lambert, ameteuliwa kuwa Rais wa muda wa nchi hiyo siku chache baada ya mauaji ya kutisha dhidi ya Rais wa nchi Jovenel Moise.

Wajumbe wa Baraza la Seneti la Haiti wamemchagua kwa kura nyingi Joseph Lambert na kumpa jukumu la kuiongoza kwa muda nchi hiyo na anatarajiwa kuapishwa ili aanze kuiongoza rasmi nchi hiyo katika kipindi cha mpito.

Vyombo mbalimbali vya habari Jumatano iliyopita vilimnukuu Waziri Mkuu wa Haiti, Claude Joseph akithibitisha kutokea shambulio na mauaji dhidi ya Rais Jovenel Moïse na kusema kuwa limefanywa na makomandoo waliokuwa na silaha kwa kusaidiwa na mamluki kutoka nje ya Haiti.

Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na mataifa mbalimbali yametoa taarifa yakilaani mauaji dhidi ya Rais Jovenel Moise wa Haiti, aliyeuawa Jumatano iliyopita kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa nchi hiyo Port-au-Prince.

Wakati huohuo watu 17 wamekamatwa wakishukiwa kuhusika na mauaji ya rais wa Haiti Jovenel Moïse.

Maafisa wa serikali ya Haiti walisema washukiwa wawili wana uraia wa Marekani na Haiti huku wengine wakiwa ni raia wa Colombia.

Serikali ya Colombia ilisema miogoni mwa washukiwa  waliokamatwa, sita  walihudumu kama maafisa wa jeshi la nchi hiyo.

Taarifa ziliongeza kwamba washukiwa wengine wanane bado wanasakwa na wengine watatu wameuliwa na polisi.

Mkuu wa idara ya kitaifa ya polisi nchini Colombia Jenarali Jorge Luis Vargas Valencia, amesema kuwa rais wa nchi hiyo Ivan Duque ameagiza utawala wa jeshi nchini humo pamoja na polisi kushirikiana katika uchunguzi huo.

Bado haijafahamika mara moja nani hasa aliye aliyehusika katika mauaji ya rais wa Haiti na kwa lengo gani.