DAMESKI, SYRIA
RAIS wa Syria Bashar Assad ametoa amri ya kuwapa maelefu ya watumishi wa umma na wanajeshi nyongeza ya mshahara ya asilimia 50 wakati nchi hiyo bado ikiwa na hali ngumu ya kiuchumi na mgogoro wa kifedha pamoja na ongezeko la bei za bidhaa muhimu.
Uamuzi wa Assad unakuja siku moja baada ya serikali ya nchi hiyo kuongeza maradufu bei ya mkate ambao ndio chakula cha kawaida nchini humo na ongezeko la asilimia 180 la bei ya mafuta ya diseli.
Agizo la rais sasa linaweka kiwango cha chini cha mshahara wa mwezi kuwa dola 22, Amri hiyo pia inawapa wanajeshi na raia wanaolipwa pensheni ongezeko la asilimia 40 katika malipo ya kustaafu.
Uchumi wa Syria umeathirika vibaya kutokana na muongo mmoja wa vita , vikwazo vya mataifa ya Magharibi, ufisadi na mzozo wa kiuchumi na kifedha wa hivi karibuni katika taifa jirani la Lebanon.
Ongezeko la mwisho la mshahara lilitangazwa mnamo Novemba mwaka 2019.