SAN SALVADOR, EL SALVADOR

WAENDESHA mashitaka nchini El Salvador wamesema wamemshitaki rasmi rais wa zamani wa taifa hilo Sanchez Caren na maofisa wengine tisa wa zamani kwa makosa ya kujitajirisha kwa namna haramu na utakatishaji fedha.

Mashitaka hayo yanahusishwa na uhalifu ambao unatajwa kufanywa na Sanchez akiwa makamo wa rais, chini ya uongozi wa Rais Mauricio Funes katika kipindi cha miaka ya 2009 na 2014.

Sanchez aliondoka nchini humo Disemba na hajarejea hadi sasa.Watuhumiwa wengine tisa pia walikuwemo katika serikali ya Funes, na wanatuhumiwa kuhusika na mpango wa malipo haramu ya kupita kiasi.

Mpango huo unadaiwa kuhusisha ubadhirifu wa kiasi cha fedha za serikali dola milioni 351.

Kwa pamoja na Funes na Sanchez walikuwa wanachama wa chama cha FMLN, ambacho kilianzisha vita vya msituni, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1980 na 1992.