CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema ghasia zilizosababisha mauaji nchini humo hazijawahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Machafuko hayo yamesababishwa na maandamano ya wiki nzima kupinga hatua ya rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kufungwa miezi 15 gerezani.
Akilihutubia taifa jana usiku, Ramaphosa amesema baadhi ya maeneo ya Afrika Kusini yanakabiliwa na siku kadhaa za vurugu, uharibifu wa mali na uporaji ambao haujawahi kutokea katika historia ya demokrasia ya nchi hiyo.
Ramaphosa amesema ghasia hizo zimevuruga mpango wa kutoa chanjo ya virusi vya corona na kwamba zitazidisha umasikini, kukosekana kwa ajira na watu kupoteza maisha.
Taarifa zinaeleza kuwa hadi hivi sasa watu 10 wameuawa, wengine wakiwa na majeraha ya risasi waliyopata baada ya jeshi kupelekwa kwenye maeneo kadhaa ya nchi ili kutuliza fujo hilo, pia watu 489 wamekamatwa na jeshi hilo.
Ramaphosa amesema aliamuru jeshi lipelekwe kuwasaidia polisi kukabiliana na waandamanaji.