CAPE TOWN, AFRIKA KUSINI

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema hakuna sababu ya kufanya vurugu kupinga hatua ya kufungwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.

Ramaphosa amesema ghasia zinavuruga juhudi za kuujenga uchumi wa nchi hiyo wakati ambapo nchi inakabiliwa na janga la COVID-19.

Amesema ingawa kuna walioumizwa na wenye hasira kwa sasa, hakuna uhalali wowote wa kufanya vurugu wala uharibifu wa mali.

Inaelezwa kuwa ghasia zilizuka kwenye miji kadhaa ya Afrika Kusini kupinga kifungo cha Zuma cha miezi 15 gerezani.

Vurugu hizo zimeshuhudiwa zaidi kwenye jimbo la KwaZulu-Natal na kuenea hadi kwenye jimbo la Gauteng na jiji la Johannesburg.

Waandamanaji walipora maduka na kuzuia barabara wakati wakiandamana kwenye miji hiyo.