NA ASYA HASSAN

SERIKALI ya Mkoa wa Kusini Unguja imesema itahakikisha inaongeza ukusanyaji wa mapato ndani ya mkoa huo ili kuisaidia upatikanaji wa fedha zitakazotumika katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Mkuu wa mkoa huo Rashid Hadid Rashid, alisema hayo ofisini kwake Tunguu, wilaya ya Kati Unguja, alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za mkoa huo kwa vyombo vya habari tangu serikali ya awamu ya nane ilipoingia madarakani.

Alisema hatua hiyo inawezekana kutokana na mkoa huo kuwa vyanzo mbalimbali vya mapato, hivyo kinachohitajika ni kila mtendaji kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, uadilifu na kuweka usimamizi mzuri wa makusanyo hayo.

Alifahamisha kuwa lengo la makusanyo kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Juni ya mwaka huu kwa wilaya ya Kati lilikuwa milioni lakini lengo hilo limevuka na kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 7.

“Tutaendelea kudhibiti mianya yote ya upotevu wa fedha hizo ili kuona makusanyo hayo yanaongezeka siku hadi siku,” alisema.

Sambamba na hayo alisema serikali imejiwekea malengo ya kuimarisha huduma mbali mbali kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji safi na salama, skuli, afya na huduma nyengine mambo hayo hayawezi kufanikiwa bila ya kuwepo fedha za kutosha.

Akizungumzia migogoro ya ardhi, Mkuu huyo wa mkoa alisema wameweza kuipunguza migogoro hiyo kwa kiasi fulani kutokana na jitihada mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na wadau mbali mbali wa sekta ya ardhi na taasisi za mkoa huo.

Alifahamisha kwamba walipoingia ndani ya mkoa huo, kulikuwa na migogoro isiyopungua 125 kati ya hiyo baadhi yake ilikuwa mahakamani na migogoro 43 imetatuliwa na mengine wanaendelea kuifanyia kazi.

“Sababu kubwa ya kuwepo kwa migogoro hiyo ni baadhi ya watendaji kutokuwa waadilifu katika kazi zao kwani unaona eneo moja linatolewa hati zaidi ya moja,” alisema Hadid.

Akizungumzia kuhusiana na hati za ardhi zilizotolewa kipindi karibu na uchaguzi mkuu, alisema wana hati 49 ambazo wanazifanyia uchunguzi na watapojiridhisha watachukua hatua zaidi juu ya maeneo hayo.