NA MADINA ISSA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewataka wananchi wa Mkoa huo na maeneo jirani kuthamini jitihada zinazochukuliwa na serikali juu ya kutoa elimu ya ujasirimali kwa makundi mbali mbali hususan vijana kwa lengo la kujikamua na maisha.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki moja ya ‘summer camp’ yaliyoandaliwa na jumuiya isiyo ya kiserekali, Perspective Devolopment Skills (PDS) kwa kushirikiana na Jumuiya ya kimataifa ya ‘HAVE A DREM’ kutoka nchini Misri, mafunzo ambayo yalifanyika Kibele Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema lengo la serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi zenye dhamira ya kuwapatia elimu vijana, kinamama na watu wenye mahitaji maalum ni kuona makundi yote nchini yanapatiwa mafunzo hayo.

Alisema mafunzo hayo yatapunguza kuwepo kwa wimbi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira pamoja na kuondokana na utengemezi katika jamii.

“Dhamira yetu serikali kutafuta wadau mbali mbali ni kuwasaidia wananchi wetu hivyo tutaendelea kutafuta wafadhili, ili muweze kufaidika na rasilimali zilizokuwepo katika nchi yenu na muweze kufanya kazi ili mujipatie riziki zenu wenyewe” alisema.

Aidha alisema kuwa vijana ndio nguvu kazi ya taifa hivyo, aliwataka kuyatumia ipasavyo mafunzo hayo na kuwawezesha kubuni miradi mbalimbali ambayo itasaidia kujipatia kipato na kujikimu kimaisha, sambamba na kujikita katika suala la kujiajiri wenyewe bila ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Khamis Abdallah Sad, alisema serekali ya awamu ya nane imetenga shilingi bilioni saba kwa kuwawezesha na kuwasaidia vijana.