ZASPOTI
MISRI itakosa huduma za nyota wa Liverpool, Mohamed Salah na mshambuliaji wa Galatasaray, Mostafa Mohamed kwenye michezo ya Olimpiki huku kocha Shawki Gharib, akitangaza kikosi cha mwisho.
Shawki amewataja mabeki wawili na kipa kama wachezaji wake waliozidi umri wa miaka 23 kwenye michuano hiyo.
Shirikisho la Soka la Misri (EFA) lilifanya majaribio ya mwisho kutaka Salah na Mohamed wapatikane kwa ajili ya Olimpiki, lakini, Liverpool na Galatarasaray walikataa maombi yao.
Tofauti na michuano ya FIFA, klabu hazilazimiki kutoa wachezaji wao kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki. Salah alikuwa mmoja wa nyota wa Misri walipofika kwenye robo fainali ya Olimpiki mnamo 2012 huko London.
Gharib badala yake alichagua kuwachukua mabeki wawili wa kati wa Zamalek, Mahmoud El-Wensh na Ahmed Hegazy mwenye makazi yake Jeddah na vile vile kipa wa Ahly, Mohamed El-Shennawi.
El-Shennawi atashiriki mechi ya fainali ya Ahly ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mnamo Julai 17, baada ya hapo amepangwa kuungana na wachezaji wenzake wa Misri huko Tokyo.
Orodha ya Misri pia ilijumuisha nyota wa Pyramids, Ramadan Sobhi, nyota aliyewika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya U23 ya Mafarao mnamo 2019 na mchezaji mwenzake, Ibrahim Adel, winga anayetamba ambaye anafanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Misri.
Kukosekana kwa mshambuliaji wa Galatasaray, Mostafa Mohamed, mshambuliaji anayecheza kwa mkopo Ceramica Cleopatra, Ahmed Yasser Rayan, anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Misri.
Gharib pia aliwataja kiungo wa Zamalek, Emam Ashour na beki wa pembeni wa Ahly Ahmed Ramadan na winga, Taher Mohamed Taher kwenye kikosi chake.
Misri itacheza katika kundi ‘C’ la michezo hiyo ya Tokyo pamoja na miamba Hispania na Argentina na vile vile Australia.
Kikosi kamili kinaundwa na walinda milango, Mohamed El-Shennawi (Ahly), Mohamed Sobhi (Ismaily) na Mahmoud Gad (Enppi).
Walinzi ni Mahmoud El-Wensh, Ahmed Aboul-Fotouh, Mohamed Abdel-Salam (Zamalek), Ahmed Hegazy (Ittihad, Saudi Arabia), Karim Fouad (Enppi), Ahmed Ramadan (Ahly), Osama Galal (Pyramids) na Karim El-Eraqi (Masry).
Viungo ni pamoja na Akram Tawfik, Nasser Maher, Taher Mohamed Taher (Ahly), Ammar Hamdi (Ittihad), Emam Ashour (Zamalek), Ramadan Sobhi, Ibrahim Adel (Pyramids) na Abdel-Rahman Magdi (Ismaily).
Washambuliaji ni Ahmed Yasser Rayan (Ceramica Cleopatra), Salah Mohsen (Ahly) na Nasser Mansi (Talae El-Geish). (AhramOnlineSports).