NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaongoza viongozi wa serikali, wa dini, wanasiasa, vyombo vya ulinzi, waandishi wa habari na wasanii waliojitokeza katika uzinduzi wa chanjo ya ugonjwa wa corona.

Uzinduzi wa chanjo hiyo ulifanyika jana ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza Tanzania kuzindua, ambapo Rais Samia alikuwa wa kwanza kupewa chanjo hiyo akifuatiwa na waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa na viongozi wengine.

Samia alisema ‘mimi ni mama wa watoto wanne wanaonitegemea, ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaonipenda sana na mimi nawapenda sana, ni mke pia lakini mbali ya yote ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi wa nchi hii”, alisema.

Alisema asingejitoa akajipeleka katika kifo wakati ana majukumu yanayomtegemea kama mama, kama bibi, kama mke, kama Rais, kama Amiri Jeshi Mkuu, lakini ameonesha umma unaomfuata nyuma akijua kuwa Rais ni mchungaji wa watu wengi.

“Ndugu zangu kama nilivyosema chanjo ni hiari ya mtu, lakini pia chanjo ni imani na inanikumbusha miaka ya 60 wakati nipo skuli ya msingi tulichanjwa chanjo karibu sita au tano na nimekuwa nikiishi nazo na zimenipa uzima wa kutosha mpaka leo nimefika hapa”, alisisitiza.

Alisisitiza kuwa, amepiga chanjo hiyo kwa hiari yake akijua kwamba ndani ya mwili kuna chanjo kadhaa ambazo zimemsaidia kumpatia maisha ya afya njema na uzima kwa muda wake wote huo.

Alisema chanjo zilizopo ni kidogo sana ikilinganishwa na idadi ya watanzania, hata hivyo jitihada zinafanywa kuhakikisha chanjo hizo zinaingia kwa wingi hapa nchini.

Samia alisema Umoja wa Afrika kwa umoja wao wameshatenga fungu la fedha la kununua chanjo na nchi za Afrika wananunua kwa AU, ambapo tayari wameshaweka oda.

Alisisitiza serikali itahakikisha inapata idadi kubwa ya chanjo ili wananchi wake waweze kupata chanjo hiyo na kuwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari.