NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, jana amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika (Africa CDC), Dk. John Nkengasong.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika ikulu jijini Dar es Salaam, Dk. Nkengasong alimpongeza Rais Samia kwa hatua anazochukua katika kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 na kusema kuwa Africa CDC inaunga mkono jitihada hizo.

Alisema Africa CDC, imedhamiria kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ikiwemo Tanzania kuweka mipango ya pamoja na kutumia fursa zinazopatikana kupitia kituo hicho katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chanjo na usambazaji wake.

Aidha, Dk. Nkengasong alisema Africa CDC wameanzisha mpango wa safari za kuaminika (Trusted Travel) utakaowawezesha wanachama wa AU kusafiri ndani na nje ya bara la Afrika bila vikwazo vitokanavyo na ugonjwa wa UVIKO 19.

Dk. Nkengasong alitaja maeneo mengine ambayo Africa CDC inaweza kushirikiana na Tanzania kuwa ni kuzijengea uwezo maabara na wataalamu ili kuimarisha upimaji na utambuzi wa aina mbalimbali za virusi vya UVIKO 19.

Aliongeza kuwa Africa CDC kupitia Jukwaa la UVIKO 19 litaziwezesha nchi za Afrika kununua bidhaa za kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa pamoja. Kupitia kikosi kazi maalum, Africa CDC inakusudia kufanya manunuzi ya pamoja ya chanjo zote zinazohitajika katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

Kwa upande wake Rais Samia alimshukuru Dk. Nkengasong kwa uamuzi wake wa kuja Tanzania kwa lengo la kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali na kumjulisha kuwa tayari Tanzania ina kamati ya kitaifa inayoratibu masuala yote yanayohusu ugonjwa wa UVIKO 19.

Rais Samia alisema mbali na kamati hiyo, serikali imeimarisha huduma za afya kwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19.

Katika mazungumzo hayo Samia alisema Tanzania imejiunga na mpango wa Covax (Covax facility) kwa lengo la kunufaika na fursa zitokanazo na mpango huo ikiwemo upatikanaji wa chanjo.