NA MWAJUMA JUMA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali inathamini mchango wa vyama vya ushirika katika kuimarisha hali za maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla kwenye maadhimisho ya siku ya vyama vya ushirika duniani yaliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil.
Alisema ustawi wa vyama hivyo haujafikia kiwango cha kuridhisha ikilinganishwa na vyama kama hivyo vya nchi jirani hivyo jitihada zichukuliwe katika kuviimarisha zaidi.
Hata hivyo alieleza kuwa hayo yatawezekana iwapo viongozi watatekeleza misingi ya utawala bora, uwajibikaji, haki na uadilifu.
Hivyo aliitaka wizara inayoshushulika na masuala ya vyama vya ushirika kuongeza kasi ya kuvijengea uwezo, kuvikaguwa na kuvisimamia vyama hivyo ili vitowe na kuondosha manung’uniko ya wanachama.
Sambamba na hayo alisema serikali imedhamiria kuimarisha matumizi ya teknolojia za habari (TEHAMA), katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi na vyama vya ushirika ili kusaidia kuleta msukumo wa jamii kutumia teknolojia hizo.
Alifahamisha kwamba katika hatua za kuimarisha vyama vya ushirika inawalazimu kuhimiza matumizi ya teknolojia ya habari katika uendeshaji wao hatua ambayo itasaidia kupata taarifa sahihi zenye uhakika, kujifunza kutoka kwa wengine na kudhibiti mapato ya wanachama.
Kuhusu suala la ombi la kuimarisha mtaji wa taasisi yao ya fedha inayotarajiwa kuwa Benki ya Ushirika Zanzibar, ili kuvipa vyama vya ushirika fursa za kushiriki katika uchumi wa buluu, alisema serikali inayafanyia kazi masuala hayo kwa kuangalia namna itakavyoweza kutatua changamoto hiyo.
Akizungumzia uchumi wa buluu, Dk. Mwinyi alisema serikali imedhamiria kuingia katika uchumi huo kwa lengo la kutumia rasilimali zilizopo baharini kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini.
Hivyo alivitaka vyama vya ushirika kushirikisha makundi yote yaliyomo katika jamii, yakiwemo makundi ya vijana, watu wenye mahitaji maalumu, wanawake na wazee, ili kufikia malengo hayo.
Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema vyama vya ushirika ni taasisi muhimu za kiuchumi ambapo inakisiwa asilimia 20 ya nguvu kazi imejiajiri au kuajiriwa kupitia vyama hivyo.
Alisema vyama hivyo hulipa kodi na kupanga mipango mbali mbali ambayo inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi na vinatoa mchango mkubwa katika kukuza demokrasia haki za binadamu, usawa, kuimarisha ustawi na kulinda amani na utulivu katika nchi yao.
Mapema akisoma risala Katibu wa Muungano wa Vyama Ushirika Zanzibar (CUZA) Suleiman Mbarouk, alisema nidhamu ya fedha, uendeshaji na usimamizi vitaendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa wanasimamiwa vyema na kupewa ushauri muafaka na Idara ya Maendeleo ya Ushirika.
Hata hivyo alisema wapo tayari kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kwenye maeneo tofauti ikiwemo kilimo cha mboga mboga, ufugaji wa samaki, majongoo, uzalishaji wa chumvi, uvuvi wa dagaa na kuendeleza kilimo cha nchi kavu, sambamba na kuendeleza uzalishaji wa uchumi wa buluu.
Sambamba na hayo walitoa malalamiko yao ikiwemo kutaka kurejeshewa eneo la Bambi Matora lililochukuliwa na JKU, ambalo lilikuwa likitoa ajira kwa vijana wengi kupitia shughuli za uzalishaji.
Siku ya Ushirika duniani huadhimishwa kila ifikapo Jumamosi ya mwanzo ya Julai ambapo kauli mbiu yake ni ‘Kwa pamoja tujenge ushirika’.