NA ZAINAB ATUPAE

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvu Zanzibar, Abdalla Hussein Kombo, amesema watahakikisha wanazifanyia kazi changamoto zinazo wakabili wakulima wa zao la Mwani.

Hussein aliyasema hayo huko Forodhani Park Mkoa wa Mjini Magharibi, katika maazimisho ya sita ya siku ya Kongano la mwani Zanzibar.

Akizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima hao, alisema ni pamoja na kukosa soka la uhakika la kuuzia biashara zao, lakini serikali inatambua changamoto hiyo na wanaendelea kuifanyia kazi.

Alisema katika kuinua biashara hiyo ya mwani serikali inashirikiana na wadau mbali mbali wandani na nje ya nchi wa sekta binafsi na kuanzisha kiwanda cha kusarifu wa zao hilo  huko Chamanangwe Pemba.

“Tunafanya hivyo hatutaki kuendelea kusafirisha mwani wetu kama mali ghafi,”alisema Hussein.

Pia alisema alifurahishwa na kitendo kilichofanywa na wadau wa Kongano hilo  kwa kushirikiana na wadau wengine kutoka Tanzania Bara kwa lengo la kubuni miradi mbali mbali, ili kuinua zao hilo ikiwemo mafunzo ya ukulima bora na usarifu wa zao hilo.

“Nilifurahishwa sana baada ya kupata taarifa kuwa Kongano hilo kilishirikiana na mashirika mbali mbali kama vile UNIDO, FAO, na Milele Zanzibar Faundation,  kuwa wameandaa siku maalumu ya zao hilo kwa lengo la kutoa fursa  kwa jamii  kujua matumizi ya zao hilo na kulifanya litumike zaidi hapa nchini  na kuongeza masoka ya ndani, ili kupunguza utegemezi mkubwa wa soko la nje,”alisema.