NA MADINA ISSA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema inaendelea kuimarisha mazingira bora ya wawekezaji, ili wawekezaji kutumia fursa hiyo katika kuwekeza kupitia sekta ya viwanda.

Akifungua semina ya uhamasishaji wadau juu ya matumizi ya falsafa, Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dr. Islam Seif Salum, alisema lengo la kufanya hivyo ni kuufanyia kazi mkakati wa kukuza uchumi wa ndani

Alisema katika kuzingatia mkakati wa kupunguza umaskini kwa wananchi na kuongeza pato la taifa hakuna budi kutafuta njia bora za kisasa zitakazoweka mifumo rasmi ya uchumi kupitia viwanda na biashara jambo litakalorejesha hadhi ya Zanzibar kuwa kituo bora cha biashara.

Sambamba na hayo, Dk. Seif, alifahamisha kuwa ili mipango hiyo itekelezeke lazima ushirikishwaji wa wananchi pamoja na sekta binafsi una mchango mkubwa na ni vyema kuyatambua  mambo yaliyozisaidia nchi nyengine kupiga hatua ikiwemo Japan, ili kuandaa sera itakayowaongoza katika kuelekea uchumi huo.

Nae Mkufunzi Mkuu wa dhana ya Kaizen, Sempeno Manongu Nyari, akifafanua dhana hiyo, alisema ni mkakati unayotekelezwa katika nchi 16 za sekta ya viwanda vyenye ubora na tija endelevu kwa kupunguza gharama za uzalishaji kupitia matumizi ya raslimali zilizopo nchini.

Semina hiyo ya siku moja iliyoshirikisha watendaji wa sekta za binafsi na serikali Zanzibar imetayarishwa na Wizara ya biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).