NA ASMA OTHMAN, IDARA YA MISITU

IDARA ya Maendeleo ya Misitu, imepiga marufuku kuingia katika hifadhi ya Msitu katika kijiji cha Mzuri, baada ya baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtende  kuvamia katika eneo hilo .

Akizungumza na Wanakamati wa vijiji hivyo, katika kikao cha usuluhishi wa mgogoro iliyojitokeza hivi karibuni, katika Ofisi Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Mkurugenzi Idara ya Misitu, Said Juma Ali, alisema ni vyema wananchi wa maeneo hayo kuacha migogoro na kujenga ushirikiano katika kuhifadhi msitu huo.

Mkurugenzi huyo aliwataka wanakijiji hao kuachana na tabia ya kulumbana na badala yake waendelee kushirikiana katika uhifadhi wa maliasili ya misitu, ili waweze kufikia malengo yaliokusudiwa.

Amefahamisha kuwa kwa kawaida migogoro hua inarudisha nyuma maendeleo ya Nchi, hivyo inapotokezea hawana budi kukaa chini na kuweka sawa tafauti zao kufanya hivyo kutawawezesha kufikia malengo yao.

Aidha, amefahamisha kuwa vijiji vyote viwili vinatakiwa kujua maeneo ya mipaka yao, ili kuwawezesha kuepuka migogoro inayotokezea mara kwa mara, kwani imebainika kutojua mipaka ya maeneo ndio sababu inayopelekea kuwepo kwa tofauti baina yao.

Akizungumzia kuhusiana na uwekezaji katika maeneo ya hifadhi ya misitu, amefahamisha maeneo hayo yapo kwa ajili ya uhifadhi na uwekezaji, hivyo si ruhusa kwa mtu yeyote kuchukua sheria mikononi mwake bila kufuata utaratibu uliowekwa.