NA SAIDA ISSA, DODOMA

WIZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh Bilioni 149 kugharamia bima za afya kwa wananchi wasio na uwezo hali itakayoboresha  huduma za afya nchini.

Aliyasema hayo wakati akizindua Bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Maadhimisho ya miaka 20 ya NHIF.

“Serikali  imepanga kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote na kuwahakikishia wananchi wote huduza za afya wakiwemo wasio na uwezo wa kugharamia matibabu, sheria hii inalenga kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na bima ya afya na kwamba kutokuwa na fedha au uwezo wa kuchangia huduma za matibabu isiwe kikwazo cha mwananchi kupata huduma za afya,”alisema Gwajima.

Aidha, alisema katika bajeti hiyo mpya ambayo utekelezaji wake umeanza Julai 1, Serikali ya Rais Samia itaendelea kuboresha sekta hiyo muhimu kwa mustakabali wa maisha ya Watanzania.

“ Utekelezaji wa jambo hili unaenda vizuri na kama mlivyomsikia Waziri Mkuu alipokuwa akisoma hotuba ya kuwasilisha hoja ya kuhitimisha bunge alisema serikali imejipanga kuwasilisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote kwenye bunge la Septemba mwaka huu,”alisema.