NA SUMAIYYA OTHMAN, PEMBA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imedhamiria kuwawezesha Vijana kwa kuwapatia vifaa na fursa mbali mbali za ujasiriamali, ili waweze kujiajiri na kupunguza wimbi la umaskini kwa kundi hilo.

Mkuu wa wilaya ya Chake chake, Abdalla Rashid Ali, alisema hayo huko Pujini Pemba , wakati akikabidhi vifaa vya kusarifu matunda na utengenezaji wa sabuni na mapambo mbali mbali kwa vikundi vinne (4) vya ushirika, kwa vijana 40 shehia ya Matale , Wara , Kichungwani na Ole. Wilayani humo.

Alieleza kuwa Serikali kila inapopata fursa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali imekuwa ikitowa vifaa mbali mbali kwa kundi la vijana ambalo ndilo kubwa tafauti na mengine kwa nia ya kumuwezesha kijana aweze kujitegemea.

Aliwataka vijana hao kuvitunza, kuvithamini na kuvitumia vifaa hivyo ili kufikia lengo lililokusudiwa  kwa kuzalisha bidhaa bora na salama kwa matumizi ya binaadamu ili kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.

“ Nawaomba nyinyi vijana ambao mumejikusanya pamoja kupitia vikundi vya ushirika , muvithamini vifaa hivi kwa ajili ya kuvitumia ilivyokusudiwa , hizi ni pesa za wavuja jasho ambao wameona kuna umuhimu wa kuwasaidia nyinyi”,alisisitiza.

Alifahamisha ili kuenda sambamba na na maendeleo ni lazima  vijana wajitambue pale  wanapo wewezeshwa na  kupatiwa vifaa vya ujasiriamali kuvifanyia kwa malengo kwani  kutawafanya wajiwezeshe na kuweza kujiajiri wenyewe na kutobweteka kusubiri ajira Serikalini.

Aidha mkuu wa wilaya ya Chake chake ,alizishukuru taasisi ya SMIDA ,UNDP , Ofisi ya Makamo wa Pilii wa Rais  pamoja na uongozi wa wilaya kwa kutoa mafunzo hayo kwa vijana hao kwani vijana ni nguvu kazi ya Taifa.

Nae  Mratibu wa  mradi huo, Edmund Mbigili kutoka UNDP alisema,kupatiwa taaluma kwa vijana hao kutaleta faida kubwa   kwanikutapunguza vitendo viovu kwa jamii na kuweza vijana kujiajiri wenyewe.