NA MWANDISHI WETU

CHAMA Cha Mapinduzi, kimesema kinahitaji kuona mipango ya Serikali yenye kuleta majawabu kwa vitendo badala ya kutumia muda mwingi kuwa na mipango inayoanisha malengo mazuri kwa kila mwaka, lakini utekelezaji wake ni mdogo.

Kimebainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameshaonesha njia na utayari wa kuwa mkombozi wa changamoto za kiuchumi pamoja na ajira kwa Vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu.

Alisema kutokana na hilo ni lazima aungwe mkono sio kwa maneno bali kwa mipango na mikakati inayotekelezeka kivitendo.

Akizungumza na wadau 28 kutoka katika taasisi za Uwezeshaji nchini,  Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Shaka Hamdu Shaka, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Takwimu Dodoma.

Alisema wakati umefika kuweko na mpango shirikishi kwa wadau hao na uwekewe utaratibu mzuri wa kufanyiwa tathimini kila baada ya muda.

“Kizazi cha miaka ya 1960 kilikuwa na wajibu wa kuleta uhuru kwa nchi yetu, kizazi baada yao  na sisi tukiwemo tunao wajibu wa kuleta uhuru wa kiuchumi na kuhakikisha nchi yetu inajenga uchumi wa kisasa ambao sio tegemezi kupitia Mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda kwa kutumia teknolojia, kazi kwetu kuamua kutekeleza wajibu huo au kuusaliti” Alisema Shaka.