MOGADISHU, SOMALIA

WATU 13 wameuawa na wengine kujeruhiwa baada ya gari lililotegwa bomu kuripuka katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Duru za usalama za Somalia zimetangaza kuwa, watu wanne wakiwemo askari polisi na raia wameuawa katika shambulio la bomu lililotegwa garini ambalo lilikuwa limemlenga Farhan Mahmoud Qarwali, mkuu wa polisi ya eneo la bandari lililoko karibu na mji wa Mogadishu.

Kwa mujibu wa duru hizo za usalama, Qarwali amenusurika katika shambulio hilo ambalo limejeruhi pia watu wengine tisa wakiwemo askari polisi na raia.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab limetangaza kuhusika na shambulio hilo likidai kwamba watu wote wanne waliouawa walikuwa askari walinzi wa kamanda huyo wa polisi.

Kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, limekiri kuhusika na hujuma za kigaidi zikiwemo za utegaji mabomu na mashambulio ya kushtukiza ndani ya Somalia na katika nchi jirani.

Al-Shabaab lilianzisha hujuma na mashambulio mwaka 2007 kwa madhumuni ya kuiangusha serikali kuu ya Somalia.

Mnamo mwaka 2011 jeshi la Somalia likishirikiana na vikosi vya majeshi ya nchi za Afrika AMISOM lilifanikiwa kuwatimua wanamgambo wa Al-Shabaab katika mji mkuu Mogadishu, lakini wanamgambo hao wa kundi hilo la kigaidi bado wanashikilia maeneo mengi ya vijijini.