ABUJA, NIGERIA

OFISI ya Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria iliripoti taarifa ya kutolewa hukumu ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa, ofisi ya Sheikh Zakzaky ilitangaza mahakama katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria imewafutia tuhuma zote zilizokuwa zikiwakabili Sheikh Zakzaky na mkewe na kuamuru kuachiwa huru.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wataachiwa huru karibuni.

Hukumu hiyo inatajwa kama ushindi kwa kambi ya muqawama mkabala wa ukandamizaji na dhulma kubwa ya serikali ya Nigeria.

Serikali ya Nigeria hadi sasa imezuia kuachiwa huru mwanazuoni huyo wa Nigeria na mkewe kwa visingizio mbalimbali na hata kuwanyima ruhusa ya kwenda kupatiwa matibabu.

Katika miezi ya karibuni ambapo hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky ilizidi kudhoofu taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zilitoa mwito mara kadhaa zikitaka kuachiwa huru Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni Disemba 13 mwaka 2015 wakati jeshi la Nigeria liliposhambulia Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria nchini humo.

Siku hiyo jeshi la Nigeria lilifyatulia risasi waumini waliokuwa katika nyumba ya mwanazuoni huyo na kuwauwa mamia ya watu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky.