NA ASIA MWALIM
MRAJISI wa Asasi za Kiraia (NGOs) Zanzibar, Ahmed Khalid Abdallah, amesema kukamilika kwa sheria mpya ya kusimamia kutaimarisha utendaji wa kazi za jumuiya hizo.
Aliyasema hayo wakati kikao cha kujadili rasimu ya mswaada wa mabadiliko ya sheria hiyo, hafla iliyofanyika ukumbi wa Kariakoo ZSSF, Zanzibar.
Alisema sheria hiyo itaanzisha bodi ikiwa ni chombo muhimu cha kuunganisha serikali na jumuiya hizo kwa kukaa pamoja na kushauri njia bora za kuziendeleza taasisi hizo.
Alisema asasi kupitia chombo hicho, zitaweza kujisimamia wenyewe kwa lengo la kuimarisha na kukuza shughuli mbali mbali za utendaji wao sambamba na kupata maendeleo nchini.
Ahmed alifahamisha kuwa Serikali ina jukumu la kuwajengea uwezo jumuiya zisizo za Serikali ili kufikia malengo waliyopanga katika katiba zao sambamba na kupata maendelao waliyokusudia.
Alifahamisha kuwa wamefanikiwa kutoa maelezo kwa jumuiya 300 ambazo zimesita kufanya kazi na kushindwa kuwasilisha ripoti zake, kwa lengo la kuzikumbusha utendaji wa shughuli wanazotakiwa kufanya.
Alieleza kuwa changamoto zinazojitokeza katika Jumuiya hizo ni kushindwa kusoma sheria, ambayo imeelekeza misingi muhimu ya kufanya kazi kwa kufuata sera, kanuni kwa mujibu wa sheria husika.
Alieleza kuwa lengo la Serikali ni kuona taasisi hizo zinaendelea kuwepo nchini kwa misingi ya kisheria na kufuata muongozo iliowekwa ili waweze kufikia malengo husika.
Mtafiti kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Ali Salum Ali, alisema sheria namba 6 ya mwaka 1995 inakusudiwa kufutwa kutokana na kupitwa na wakati jambo linaloonekana kuwakosesha uhuru na kushirikishwa katika baadhi ya mambo muhimu kwa ustawi wa taasisi hizo.
Aidha alisema sheria inayopendekezwa imeweka vipengele na kuanzisha vyombo vitakavyoongeza ushirikishwaji wa asasi hizo kujadili mambo mbali mbali ya utendaji wao wa kazi, matatizo yanayowakumba yaweze kuwasilishwa kwa mrajisi ili aweze kuyapeleka Serikali kutatuliwa.