NA HAFSA GOLO
MKURUGENZI Mwendeshaji wa Shirika la Meli na Uwakala Zanzibar, Makame Hasnuu Makame, ameishauri serikali kufikiria kununua meli mpya ya abiria ambayo itaendana na ushindani wa soko.
Alieyasema hayo alipokua akizungumza na Zanzibarleo ofisini kwake Malindi Mjini Unguja, ambapo alisema ununuzi wa meli hiyo ni vyema uwe wenye kukidhi mahitaji ya kiwango kizuri cha matumizi ya mafuta.
Aidha, alisema hatua hiyo iwe sambamba na suala la kuajiri nguvu kazi mpya ya wazalendo ambao wenye taaluma ya elimu ya ufundi wa meli, uendeshaji na ubaharia.
“Hivi sasa wafanyakazi wengi wa shirika hili ni wastaafu hivyo tunahitaji nguvu kazi mpya iliyosomea katika fani hiyo ili kuwe na mageuzi ya kiutendaji”,alisema.
Pia Makame alisema, ununuzi wa meli ya abiria uwe unalingana na mazingira ya visiwa vya Unguja na Pemba kwa madhumuni ya utoaji huduma nafuu kwa wananchi.
“Tutaponunua meli yenye kuzingatia ushauri huo itasaidia hata pale inapotokea hitiliafu za kiufundi ama kuharibika kuwatumia fundi wa ndani baada ya kutumia fundi wa nje”,alisema. Aliongeza kuwa ununuzi wa aina hiyo wa meli utarahisisha utoaji wa huduma bora na zenye ufanisi kwa utendaji wa shirika hilo kwa safari za Unguja na Pemba.