Ni ugonjwa hatari kuliko UKIMWI

Idadi ya wagonjwa yaongezeka kila mwaka

NA MOHAMED SHARKSY (SUZA)

Hapo juzi dunia iliadhimisha siku ya ugonjwa wa homa ya ini ambapo Zanzibar nayo kama sehemu ya dunia nayo ina wagonjwa wa aina hiyo.

Homa ya Ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya virusi ambavyo vikishaingia mwilini hushambulia ini kabla ya kugeuka maradhi sugu, virusi hivyo vinaitwa HBV (Hepatitis B Virus).

Tafiti nyingi za kitaalamu zimeonesha kuwa virusi hivyo ni hatari kuliko hata vya Ukimwi kwa sababu vinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu (yaani nje ya mfumo wa damu) kwa siku saba.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiyo eneo hatari zaidi kuwa na maambukizi ya virusi vya ini ambapo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni moja ya nchi zilizopo katika eneo hilo ni moja ya nchi iliyoathirika na ugonjwa huo.

NINI INI LA MWANAADAMU

Ini (liver) ni miongoni mwa mwa kiungo muhimu katika mwili wa binadamu ambapo viungo vinavyosafisha mwili na kutoa uchafu.

Aidha ini hutumika pia katika uhifadhi wa chakula katika mwili wa binadamu na hufonzwa kuingia mwilini katika utumbo mwembamba huelekea kwanza katika ini.

Sambamba na hilo ini husafisha sumu katika mwili na kunapokuwa na ongezeko la chakula cha protini ini hurekebisha.

Uchafu unaotolewa na ini huingizwa katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na hutolewa pamoja na kinyesi.

Kwa kawaida wastani kirusi cha HBV kikishaingia mwilini, hupevuka ndani ya siku 75, hata hivyo upo uwezekano wa kupevuka kati ya siku 30 hadi 180.

Ndani ya siku 30 mpaka 60, mtu mwenye HBV anaweza kugundulika ikiwa atapimwa huku wastani mdogo wa kuishi kuliko mwenye Ukimwi.

Kwa maana hiyo, mwenye maambukizi ya Virusi vya Homa ya Ini hufariki dunia haraka kuliko mwenye VVU.

Kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa ini hapa Zanzibar, kwa makusudi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara yake ya Afya ikishirikiana mpango shirikishi wa kitengo cha ukimwi, homa ya ini kifua kikuu na ukoma imeamua kupambana na ugonjwa huo.

Kwa mukhtaza huo basi Jamii inatakiwa kuchunguza afya zao kwa kupata kipimo cha homa ya ini, ikiwemo chanjo mapema kwani mtu anaweza kupata virusi hivyo bila dalili kujitokeza.

HALI HALISI YA UGONJWA WA HOMA YA INI ZANZIBAR

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto zinasema kuwa bado kuna wimbi la maambukizi katika jamii.

Taarifa hiyo ilisema kuwa wagonjwa wa homa ya ini alisema tangu mwaka 2017 mpaka 2021 wagonjwa wanaoripoti kwa ajili ya matibabu ni 1,165.

Kati ya wagonjwa hao wanawake ni 622 na wanaume ni 640 ambazo ni takwimu ya hospitali kuu ya Mnazi mmoja pekee.

Makundi makubwa matano ambayo yako katika hatari zaidi ya kupata homa ya ini ni pamoja na wanaume na wanawake wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.

Makundi mengine ni watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano, wafanyakazi na wahadumu wa afya pamoja na wale wanaoishi na wagonjwa wanaougua ugonjwa huo.

WITO KWA JAMII

Jamii imetakiwa kufika vituo vya afya kwa ajili ya kufanya uchunguzi hasa kwa wale ambao wameshapata ugonjwa huu kuendelea kupata matibabu sahihi ili kuepukana na madhara yatokanayo na homa ya ini kama vile saratani, sonono na mwisho wake ni kifo.

Hivyo ipo haja kwa Wizara kufanya utafiti mkubwa utakaohusisha kwa watu wote wa Unguja na Pemba ili kuweza kutambuwa idadi halisi ya wagonjwa waliopo.

WAGONJWA WANASEMAJE?

Zahra Haji Mwita, mkaazi wa Magomeni ambae ni muathirika wa maradhi ya homa ya  ini kwa kipindi cha miaka mitatu sasa  alisema aliweza kugundulika na ugonjwa huu  wakati wa ujauzito wake  wa pili.

Hata hivyo, alisema kwa sasa anaendelea na matibabu katika  hospitali kuu ya mnazi mmoja.

Zahra alisema yeye ni  mtu wa tatu katika familia yao ambao ina wagonjwa  watatu jambo ambalo linaonesha kuwa alipata maambukizi kutoka kwa ndugu zake hao wa karibu.

“Ugonjwa huu niliupata baada ya kuambukizwa na mmoja kati ya ndugu zangu hao wawili na wao wote hao wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Mnazi  mmoja”, alisema.

Nae Hassan Haji Mwita, kaka wa Zahra alisema yeye ni mtu wa mwanzo kupata  ugonjwa huu   na imeonyesha  kwamba  miongoni mwa kati ya familia yake ndie aliyepata.

“Wagonjwa hawa wengine wa familia walipata maambukizi baada ya kuniuguza mimi”, alisema kwa masikitiko.

MAKUNDI HATARISHI ZAIDI YA UGONWA WA INI

 Kwa mujibu wa tafiti nyingi duniani zimeonyesha kwamba makundi hatarishi ya ya ugonjwa huu ni pamoja na watoto wachanga ambao huambukizwa katika kipindi cha mwaka wa kwanza tangu kuzaliwa ambao ni kati ya asilimia 80 na 90.

Aidha asilimia 30-50 huambukizwa kabla ya kufikisha umri wa miaka sita, huku watu wazima wanaopata HBV wakiwa ni asilimia 90.

Pia utafiti unaonesha kuwa chini ya asilimia 25 ya watu wazima walipata maambukizi utotoni na hatimaye Hepatitis B kuwa sugu jambo ambalo hufariki dunia kutokana na matokeo ya ini kuharibika kabisa au kwa saratani ya ini.

Ugonjwa huu kama haujatibiwa hutengeneza uvimbe katika ini na kusababisha saratani ya ini na baadaye Kifo.

SABABU ZINAZOPELEKEA KUPATA HOMA YA INI

Kuambukizwa kwa kufanya tendo la ndoa, kushikana na majimaji ya mwili wa mtu aliyeathirika ikiwa ni pamoja na damu, mate, machozi na mkojo.

Sababu nyengine za kuugua ugonjwa huu ni pamoja na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa.

NJIA KUU ZA MAAMBUKIZI

Kunyonyana midomo, mama mjamzito au anaenyonyesha ana uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi mapya.

Kuchangia damu isiyo salama, kuchangia vitu vya ncha kali kama sindano, kuchangia wembe, Kuchangia miswaki, kuchangia taulo na mwenye ugonjwa huo, kubadilishana nguo au kugusana wakati mkiwa mnavuja jasho.

DALILI NA ISHARA HOMA YA INI

Homa ya ini aina ya ‘B’ inaweza kuua kimyakimya bila kuonyesha dalili zozote ambapo mara nyingi sana huenda dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa na zinapoonekana tayari ini limeshanyauka au kuwa na saratani.

Dalili nyengine ni pamoja na homa kali sana na ambayo hudumu kwa kipindi kirefu, maumivu makali ya tumbo upande wa ini, kuchoka sana kwa mwili.

Kichefuchefu kwa wingi, mwili kuwa dhaifu, kutokuwa na hamu ya kula, kukonda, macho na ngozi kuwa vya njano, mkojo kuwa manano kwa weusi.

VIPIMO VYA HOMA YA INI

Kipimo cha HBsAg. hiki ni kipimo cha kuainisha iwapo umeambukizwa virusi vya homa ya ini vya HBV na je, una uwezo wa kuwaambukiza watu wengine au la?

Kipimo hiki huchunguza aina ya ‘antigeni’ ambayo ni sehemu ya nje ya virusi na kupatikana kwake kwenye damu yako humaanisha kuwa una maambukizo ya u Hepatitis B yaliyo hai na unaweza kuwaambukiza wengine kwa urahisi.

Kipimo cha HBsAg kinapokuwa ‘negative’ haina maana kuwa huna ugonjwa huo kwa asilimia 100, bali pengine virusi vimelala, uliambukizwa zaidi ya miezi 6 iliyopita au chanjo yako bado ni imara.

Aidha Kipimo cha pili cha Hepatitis B ni Anti-HBs, Kipimo hiki ni cha kuangalia iwapo mtu ana kinga ya virusi vinavyosababisha homa ya ini na iwapo mwili umetengeneza antigeni ya kupambana na ugonjwa huo. Kuwa positive kipimo hiki kunamaanisha hali mbili.

Kipimo cha tatu cha ugonjwa wa Hepatitis B ni Anti-HBc, ambacho huainisha iwapo uliwahi kuambukizwa ugonjwa huo huko nyuma au maambukizo ni ya hivi karibuni.

Kipimo hiki huangalia ‘antibodi’ inayotokana na sehemu ya ndani ya kirusi cha HBV inayopatikana kwa watu walioambukizwa ugonjwa huo. Iwapo kipimo hiki ni positive inamaanisha kuwa, kuna uwezekano una maambukizo ya muda mrefu ya homa ya ini yaliyo hai na unaweza kuwaambukiza wengine.

Vipimo vingine vya nyongeza ni HBeAg na Anti-HBe ambavyo huonesha kwa kiasi gani unaweza kuwaambukiza wengine ugonjwa huo na kiwango cha virusi vya homa ya ini mwilini.

Kwa wale wanaopatikana na maambukizo ya ugonjwa huo, vipimo zaidi hufanywa kama vile ultrasound ili kuonesha mabadiliko ya ini, kwani kama tulivyosema virusi vya Hepatitis huathiri seli za ini hivyo, baadhi ya wakati pia MRI na CT scans hufanywa ili kuangalia uvimbe katika ini kwa watu ambao virusi vya ugonjwa huo tayari vimewasababishia vidonda katika ini au kitaalamu liver cirrhosis na pia kensa.

Kipimo cha mwisho ni ‘biopsy’ ya ini ambayo kwa ujumla huonesha uzima wa ini. Kipimo hiki hufanywa ili kupata uhakika iwapo ini lina vidonda au saratani. 

MATIBABU YA UGONWA WA HOMA YA INI

Mpaka muda huu tulionao ugonjwa huu hauna tiba, vilevile hakuna dawa maalum za kurefusha maisha, ugonjwa huo ukishafikia kiwango cha ini kuharibika au kupata saratani ya ini, maana yake kinachofuata ni kifo.

Mara nyingi ugonjwa wa ini hupotea wenyewe bila ya dawa, wala mgonjwa hahitaji kulazwa hospitali, mgonjwa anatakiwa apumzike sana

Kupandikiza ini ambapo ini lililo athirika huondolewa na kuwekwa ini lingine.

KINGA DHIDI YA HOMA YA INI

Kupatiwa chanjo, chanjo hii hutolewa kwa awamu tatu, ambapo ya kwanza hutolewa mara baada ya kipimo cha Hepatitis B, ya pili hutolewa mwezi mmoja baada ya chanjo ya kwanza, na chanjo ya tatu hutolewa miezi sita baada ya chanjo ya kwanza.

Kutumia kinga wakati wa kujamiana au kuacha kabisa, kuacha kuchangia vitu vya ncha kali kama sindano, wembe, herini nakadhalika.

Kutochangia miswaki, Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu, kuacha kuchangia damu isiyo salama nakadhalika.

Hivyo ipo haja ya kujikinga na ugonjwa huu ambao ni hatari kwa maisha ya binaadamu.