NA MAULID YUSSUF, WEMA

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe, Simai Mohammed Said amesema mataifa kadhaa yapo tayari kuisaidia Zanzibar kimaendeleo ili ipige hatua ya kufikia malengo ya uchumi wa buluu hasa katika sekta ya elimu.

Alisema hayo wakati wa hafla ya kukabidhiwa msaada wa vitabu vya sayansi katika ukumbi wa wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja, ambapo alisema ili kufikia haraka malengo hayo ni vyema kuitumia misaada inayotolewa na wahisani kama ilivyokusudiwa.

Alisema nchi yoyote ili ifikie malengo ni lazima iwe na misingi imara ya elimu kwani ndio mama wa maendeleo katika kila taifa na kwamba Zanzibar ipo tayari kutoa mashirikiano na nchi mbali mbali duniani ikiwa lengo ni kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa buluu.

Aidha aliwaomba wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuhakikisha wanaisaidia Zanzibar katika nyanja zote za maendeleo.

Alisema msaada vitabu hivyo watavigawanya zaidi katika skuli zenye uhaba wa vitabu kwani kuna baadhi ya Wanafunzi wanatumia kitabu kimoja watu wawili kutokana na tatizo hilo.

Kwa upande wake   Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Profesa Hamad Rashid Hikimany amesema wametoa vitabu ili kuunga mkono masomo mbalimbali hasa ya sayansi hali ambayo inaweza kupelekea wanafunzi kuweza kufaulu vyema katika masomo hayo.

Aidha alisema malengo yao ni kuhakikisha wanatoa misaada katika kuleta maendeleo ya Taifa lao hasa sekta ya elimu kwani vitabu vya dini zote vimetilia mkazo juu ya suala la kupata na kutoa elimu.

Zaidi ya vitabu 1,000 kutoka skuli ya Langley Academy Sekondary iliopo mtaa wa Berkshire nchini Uingereza vimekabidhiwa vikiwemo vitabu vya hesabu, kemia, fizikia na kiengereza.

Wakati huo huo, waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohammed Said amefanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa China nchini Tanzania Zhang Zhisheng ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja, wakati alipofika kwa ajili ya kukabidhi  msaada wa mikoba ya Skuli kwa ajili ya kuwapatia Wanafunzi.