NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Simai Mohammed Said, amewataka wanafunzi kusoma masomo yenye tija kwa serikali ili kupata wataalamu wa kada mbalimbali nchini ikiwemo fani ya ardhi.

Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua maonesho ya pili ya elimu ya juu Zanzibar yaliyozishirikisha taasisi mbalimbali za elimu na vyuo vikuu vya Zanzibar na Tanzania bara yaliyofanyika katika uwanja wa Mapinduzi Square.

Alisema ikiwa wanafunzi wataweza kusoma fani hiyo na fani nyengine basi serikali itaweza kutoa wataalamu wenye sifa na wazalendo katika nchi.

Simai alisema Zanzibar ina uhaba mkubwa wa watalaamu wa fani hizo kama mipango miji, wapimaji, wachoraji ramani na watalaamu wengine wanaotokana na fani hiyo.

Alisema maonesho hayo yanalenga katika kujua miongozo na taratibu za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu na kupata fursa za kujua nafasi za masomo zinazotolewa nchini na nchi nyengine jirani.

Aliahidi  wizara kukifanyia ubunifu kwa kukipa nguvu Kitengo cha Elimu ya juu ili wanafunzi waweze kupata taaluma na kufaidika katika siku za mbele.

Sambamba na hayo aliwasisitiza wanafunzi hao kuhakikisha wanaenda katika taaluma zote ambazo serikali inazihitaji katika kupata wataalamu wa ndani ya nchi ili kwenda sambamba na mpango mkuu wa nchi na matarajio kwa sekta binafsi.

Waziri Simai aliwataka wanafunzi kuwa na nguvu na upeo wa kufanya kazi kupitia fani mbalimbali ili kujiwezesha kufanya kazi sehemu yoyote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Prof. Mayunga Nkunya, aliipongeza Wizara ya Elimu kwa kuyaendeleza maonesho hayo ambayo ni muhimu kwa wanafunzi katika kujiwekea malengo yao ya baadae.

Alisema maonesho hayo kwa Tanzania yameanza miaka 10 iliyopita na wameona manufaa yake hasa kwa wanafunzi kujua mambo mbalimbali katika kujiunga na vyuo vikuu na kupanua fursa za maisha hapa duniani.

Alisema tume yao ya Vyuo Vikuu (TCU) inafanya mambo makuu matatu muhimu ikiwemo kuhakiki ubora wa elimu ya juu nchini Tanzania, kutoa ushauri wa vyuo vikuu serikali za wanafunzi na jamii nzima ya Tanzania, msaada wa vyuo katika uendeshaji wa vyuo vikuu na elimu ya juu na ukuaji wa vyuo hivyo Tanzania.