NA TIMA SALEHE , DAR ES SALAAM
TIMU ya Wanawake Simba Queens inatarajia kwenda Kenya Julai 14, mwaka huu katika michuano ya kimataifa ya CECAFA Woman.
Michuano hiyo itashirikisha Mabingwa 11 wa ligi kuu za wanawake kutoka nchi mbali mbali na inatarajia kuanza Julai 17, mwaka huu.
Akizungumza na Zanzibar Leo, kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Mgosi, amesema droo ya kupanga makundi ya timu zitazoshiriki michuano hiyo inatarajiwa kufanyika nchini Kenya.
Alisema baada ya droo hiyo watajua wapo kundi gani lakini timu itaondoka Julai 14, kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwa waandaaji wa michuano hiyo.
Mgosi alisema kwamba anaimani na timu yake hivyo hahofii timu yoyote, ambayo inaweza kuwazuia wao kufanya vizuri.