NA MWANDISHI WETU

PAMOJA na kutangazwa mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara, uongozi wa klabu ya Simba umesema unahitaji  kushinda mechi zote mbili zilizobaki ikiwemo dhidi ya Azam FC.

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union juzi Simba ilitawazwa mabingwa wa ligi kuu 2020/21 kwa mara ya nne mfululizo.

Kocha Msaidizi Seleman Matola, alisema timu itaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta pointi tatu na licha ya  kutangazwa mabingwa.

“Ni kweli tumeshinda ubingwa wa ligi lakini haimaanishi tunazichukulia kawaida mechi zilizobaki. Mechi dhidi ya Azam itakuwa ngumu lakini tupo tayari kupambana kupata ushindi,” alisema Matola.

Matola amewataja nyota wanne Bernard Morrison, Jonas Mkude, Miraji Athumani na Ibrahim Ajibu ambao watakosekana kwenye mchezo wa kesho kwa sababu tofauti.

“Tutawakosa Morrison ambaye ameenda nchini kwao Ghana ana matatizo ya kifamilia, Mkude suala lake bado halijamalizika, Miraji amepata majeruhi mazoezini na Ibrahim Ajibu,” alisema Matola.